Hai, Kilimanjaro
Serikali imepata mwarobaini wa kudhibiti changamoto ya miundombinu katika eneo korofi la Kwa Msomali, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, ambalo limekuwa kikwazo kwa mamia ya wasafiri wanaotumia barabara kuu ya Moshi-Arusha.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi eneo la mradi kwa mkandarasi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa madaraja saba na kunyanyua tuta la barabara kwa kimo cha mita 1.5 katika maeneo yenye urefu wa mita 500 na 1,725.
“Eneo hili limekuwa kero kwa muda mrefu, lakini sasa serikali imepata mwarobaini wa kuhakikisha maji hayafuriki tena na magari yanapita bila kikwazo,” alisema Babu.
Mradi huo wenye thamani ya Sh5.8 bilioni unatekelezwa na kampuni ya Kings Builders ya Dar es Salaam chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads). Mkataba wa mradi huo ulisainiwa Novemba 1, 2024, jijini Dodoma, ukishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Innocent Bashungwa.
Aidha, Babu amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuimarisha uchumi wa mkoa kwa kurahisisha usafiri wa bidhaa na abiria. Pia amehimiza usimamizi madhubuti ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.
“Nawataka Tanroads kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa viwango vya juu ili barabara na madaraja yadumu kwa muda mrefu. Vilevile, wananchi wa maeneo haya wanapaswa kushirikiana kulinda mradi huu,” amesema Babu.
Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro amesema,Injinia Benitho Mdzovela amesema: “Mradi huu ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kurejesha miundombinu iliyoathiriwa na mvua za ElNino zilizonyesha kuanzia mwishoni mwa 2023. Barabara ya Himo na Kia ni mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa vibaya.”
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kia, Joseph Laitayo, ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu na kuhakikisha usalama wa vifaa vya mradi huo.
Hata hivyo, amemuomba Mkuu wa Mkoa kuhakikisha eneo hilo linapewa alama za zebra na stendi ya mabasi ili kupunguza ajali na kurahisisha huduma kwa wananchi.
Diwani wa Kata ya Kia, Tehera Mollel, amesema mradi huo ni mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakikumbwa na adha ya mafuriko na msongamano wa magari.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 10, na matarajio ni kwamba utaleta suluhisho la kudumu kwa changamoto za usafiri katika eneo hilo.