Mwenyekiti wa chama tawala cha Korea Kusini amehimiza chama chake kupiga kura kupinga hoja ya kumuondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol, inayoongozwa na upinzani. Kwa upande mwingine wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema kuwa imeongeza mawasiliano ya karibu zaidi na Marekani tangu Rais Yoon alipotangaza sheria ya kijeshi siku ya Jumanne.
Rais Yoon wa Korea Kusini bila kutarajia alitangaza sheria ya kijeshi siku ya Jumanne na saa chache baadaye tangazo hilo lililopingwa vikali hasa na upinzani nchini humo lilileta mshangao mkubwa si tu kwa raia nchini humo bali ulimwengu mzima ulipigwa butwaa na kusababisha maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.
Soma zaidi. Wabunge wa upinzani Korea Kusini kupiga kura ya kumfungulia mashtaka rais Yoon Suk Yeol
Shirika la habari la Yonhap mapema leo limemnukuu mwenyekiti wa chama tawala Han Dong Hoon akisema kwamba yeye kama kiongozi wa chama atafanya kila kitakachowezekana kuhakikisha kuwa mashtaka hayo yanayomkabili rais hayapiti bungeni ili kuzuia madhara na machafuko ambayo hayakutarajiwa kutoka kwa umma na wafuasi wa vyama.
Tukio la siku ya Jumanne la kuiweka nchi chini ya sheria ya kijeshi lilikuwa ni la mara ya kwanza tangu mwaka 1980 wakati wa serikali ya mpito nchini humo.
Kutokana na msukosuko huo, wabunge wa upinzani walitia saini ombi kwa mashauri ya mashtaka, ambayo yanapangwa kupigiwa kura na bunge siku ya Jumamosi.
Maelfu waandamana
Maelfu ya raia wa Korea Kusini wanaandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Seoul wakimtaka rais wa nchi hiyo kuwajibika kwa kujiuzulu kwa kitendo hicho cha kuiweka nchi chini sheria ya kijeshi.
Kim Jun Hyun, Mzee wa miaka 55 ambayo ni miongoni mwa waandamanaji waliojitokeza barabarani “Ikiwa Yoon Suk Yeol hatashtakiwa tunaamini kwamba kutakuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa watu kuliko hata wakati wa Park Geun-hye, na hata katika kipindi hiki cha baridi kali, raia wengi watakusanyika pamoja kuilinda demokrasia ya nchi yetu.”amesema mzee huyo.
Soma zaidi. Upinzani Korea Kusini wawasilisha mswada wa kumuondoa rais Yoon
Mbali na mzee huyu yupo pia binti wa miaka 26, Cha Ye-Ji ambaye naye anaeleza kile kilichomsukuma ajitokeze kwenye maandamano haya. “Nitaendelea kuja hapa hadi historia iwekwe sawa, na haijalishi Yoon Suk Yeol atafanya nini ili kudumisha nguvu zake, tutapinga.”
Wakati hali hiyo ya kisiasa ikiendelea kupamba moto, wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo imesema imeongeza mawasiliano zaidi na Marekani hasa katika kipindi hiki ambacho serikali ya nchi hiyo ikiwa kwenye shinikizo kubwa.
Hata hivyo, hapo jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema kwamba nchi yake haikufahamishwa mapema juu ya uamuzi wa Rais Yoon wa kuiweka Korea kusini chini ya sheria ya kijeshi.