Ebwanaee VAR kutumika CHAN 2025

KATIKA hatua ya kihistoria kwa soka la ukanda wa Afrika Mashariki, imetangazwa kuwa Teknolojia ya Video Assistant Referee (VAR) itatumika rasmi katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ya mwakani.

Tangazo hili linakuja siku chache kabla ya mashindano hayo, ambayo yatafanyika kuanzia Februari 1 hadi 28, 2025.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa matumizi ya teknolojia hii, ambayo imekuwa ikitumika katika mashindano makubwa kama vile Ligi ya Mabingwa ya Afrika tangu nusu fainali za mwaka 2021, na pia katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2023.  Awali VAR ilishuhudiwa katika fainali za Kombe la Mataifa kwa Vijana U17 zilizofanyika mwaka 2019 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Uwanja wa Benjamini Mkapa kwa Tanzania Bara na Amaan huko Zanzibar zitakuwa na mfumo wa VAR, huku vifaa vya teknolojia hii vikitarajiwa kuwasili karibuni ili kuwekewa maandalizi ya mwisho kabla ya mashindano kuanza.

Viwanja vingine ambavyo navyo vinatarajiwa kuwekewa mfumo huo mbali na hivyo vya Tanzania ni pamoja na Namboole nchini Uganda, Nyayo na Kasarani nchini Kenya. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki kuwa wenyeji wa michuano hiyo kwa pamoja.

Akiongelea hilo, Meneja wa CAF kwa mashindano ya CHAN, Serge Assume alisema kuwa vifaa vya VAR vitakamilishwa na kufanyiwa majaribio kabla ya michuano kuanza.

Teknolojia ya VAR itasaidia kuboresha ubora wa uamuzi wa waamuzi, hasa katika hali zinazohitaji uamuzi wa haraka na sahihi. Inatumika katika masuala manne makuu ya mchezo, ambayo ni Uamuzi wa goli, uamuzi wa penalti, kadi nyekundu za moja kwa moja, kufichua makosa.

Teknolojia ya VAR inajumuisha vipengele vingi, ikiwa ni pamoja na kamera zinazochukua mechi kutoka mikao mbalimbali, msaidizi wa VAR anayefuatilia mchezo, msaada wa waamuzi wa VAR, Opereta wa kurejesha video, eneo la mapitio ya waamuzi (RRA), ambapo waamuzi wataweza kupitia uamuzi wao, VAR Light na VHF Omnidirectional Range, ambavyo vinatuma ishara kutoka kituo cha ardhini hadi kwenye antena ya mfumo.

Related Posts