Fei toto: Msijali nitaendelea kutupia

KIUNGO Mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema ushindi mfululizo wanaouwapa unawajengea morali nzuri na kuhusu suala la kutupia atafanya hivyo kila akipata nafasi.

Fei Toto amehusika kwenye mabao tisa kati ya 19 yaliyofungwa na timu hiyo kwenye mechi 13 walizocheza na kufanikiwa kukusanya pointi 30 baada ya ushindi mara tisa, sare tatu na kufungwa mara moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto alisema ushindi mfululizo umewajengea kujiamini na kutengeneza muunganiko mzuri wa timu ambayo malengo yao ni kuhakikisha wanarudi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

“Licha ya mabadiliko ya benchi la ufundi kikosi kimejengeka kila mchezaji anatafuta nafasi ya kuipambania timu, inafurahisha na inatupa morali nzuri ya kujiweka kwenye ushindani,” alisema na kuongeza;

“Hatukuwa na mwanzo mzuri, sasa tumeweza kuingia kwenye mfumo wa mwalimu na tunatumia vizuri maelekezo tunayopewa kwenye uwanja wa mazoezi, hii ndio siri kubwa ya mafanikio tuliyonayo sasa.”

Fei Toto akizungumzia mchango wake ndani ya kikosi cha timu hiyo tangu amejiunga nayo akitokea Yanga alisema anafurahi kuingia ndani ya kikosi hicho na kuweza kuendana na kasi ya timu.

“Tangu nimetua ndani ya Azam FC sijisifii namba zinaongea, nafurahi kuwa ndani ya timu, nina furaha kuwa hapa na nafurahia mafanikio niliyoyaweka. Mipango ni kuona naipambania timu hii kufikia malengo ya kutwaa mataji,” alisema na kuongeza;

“Msimu huu malengo yetu kama timu ni kutwaa mataji yote tunayoshiriki lengo ni kuona tunapata uwakilishi kwenye moja ya michuano mikubwa ya kimataifa, hilo linawezekana kutokana na namna timu ilivyo na wachezaji wenye uchu wa mafanikio.”

Related Posts