Klabu ya Yanga imeweka kambi kwenye hoteli ya kifahari ya The Legacy Luxury iliyopo Hydra, Algiers, Algeria, ikiwa sehemu ya maandalizi ya mechi yao ya pili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Jumamosi Desemba 7, 2024 dhidi ya MC Alger.
The Legacy Luxury Hotel ni chaguo maarufu kwa timu za michezo na wageni wa hadhi ya juu. Hoteli hii ina vyumba 126 vilivyokamilika kwa huduma za kisasa kama mtandao wa Wi-Fi, spa, sauna, na gym. Pia, hoteli inatoa vyakula vya kimataifa.
Huduma na Gharama za Hoteli
The Legacy Luxury Hotel ina vyumba vya aina mbalimbali, vinavyokidhi mahitaji ya wageni wa hadhi tofauti. Kwa mujibu wa bei za kawaida: Vyumba vya kawaida (Standard Rooms): Vinagharimu kati ya $150 na $180 kwa usiku mmoja, sawa na TSh 412,500.
Vyumba vya kifahari (Luxury Suites): Vinagharimu wastani wa $200 kwa usiku mmoja, sawa na TSh 500,000.
Hoteli hii ipo umbali wa takribani kilomita 15 kutoka Uwanja wa Julai 5, 1962, ambapo mchezo kati ya Yanga SC na MC Alger utafanyika. Kwa wastani, safari kutoka hotelini hadi uwanjani inaweza kuchukua dakika 30 hadi 40 kwa gari.
Uwanja wa Julai 5, una uwezo wa kubeba mashabiki 76,200 na ni mojawapo ya viwanja vikubwa zaidi nchini Algeria. Unajulikana kwa mandhari yake nzuri na nyasi zenye ubora wa juu zinazofaa kwa mechi kubwa kama hizi za Klabu Bingwa Afrika.
Mechi hii ni fursa kwa Yanga kufufua matumaini yao ya kufuzu hatua ya robo fainali baada ya kupoteza mchezo wao wa awali dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwa mabao 2-0.