MTANZANIA anayecheza soka la ufukweni Morocco, Jaruph Juma, mambo yamezidi kumnyookea baada ya chama lake la Ain Diab iliyopo Ligi Kuu ya Ufukweni, kushinda kwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 2-2 dhidi ya Sbou Knetra.
Jaruph aliliambia Mwanaspoti licha ya mechi hiyo kuwa ya kawaida ya ligi, lakini namna ushindani ulivyokuwa haikutofautiana na mchezo wa fainali.
Jaruph ni Mtanzania pekee anayecheza soka la ufukweni nchini humo baada ya wiki chache kutambulishwa na klabu hiyo na juzi ilikuwa ni mchezo wa pili kwake akitumika kwa dakika zote 90, kwani alianza dhidi ya Hercules wakishinda mabao 5-0 huku akifunga hat-trick.
“Unajua kwenye soka la ufukweni hakuna sare hivyo mtapambana hadi mshindi apatikane na baada ya sare ikapigwa mikwaju ya penati tukashinda, lakini timu zote zilicheza vizuri,” alisema Jaruph na kuongeza;
“Kwenye soka la ufukweni ni ingia toka kama ilivyo Futsal, muda wa mchezo ni dakika 36 zenye vipindi vitatu na kila kipindi mapumziko dakika tatu ndiyo maana nilisema hakuna sare.”
Ukiachana na mchezo huo, lakini Jaruph aliwahi kukipiga soka la kawaida akiwa na Yanga U-20 (2015), African Lyons kuanzia 2019/21 na Simba (2016).