Timu ya maafande wa JKT imevunja ukame wa miaka saba baada ya kuibeba ubingwa wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (DB), kwa kuifunga UDSM Outsiders katika mchezo wa nne kati ya mitano ya fainali ya ligi hiyo uliopigwa kwenye Uwanja wa Donbosco Oysterbay.
Maafande hao waliwatambia wapinzani wao kwa ushindi wa jumla wa 3-1 na kubeba ubingwa ukiwa ni wa kwanza tangu ilipobeba mara ya mwisho mwaka 2018.
Msimu uliopita JKT ilikwama kubeba ndoo kwa kuzidiwa maarifa na Dar City ambayo msimu huu iliutema ubingwa mapema.
Fainali hiyo ilipangwa kuchezwa kwa michezo mitano (best of five play-off), iwapo kama Outsiders ingeibuka na ushindi juzi, kwani mchezo wa kwanza JKT ilianza kwa ushindi wa pointi 67-52, kisha zilipokutana kwa mara ya pili, Outsiders ilijibu mapigo kwa kushinda 66-55.
Kisha katika michezo miwili ilifuata, JKT kushinda mara zote kwa pointi 66-55 na 70-65 na kuifanya iwe mbele kwa 3-1 na kufanya mechi ya mwisho isichezwe na badala yake kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa DB.
Katika fainali hiyo ya tatu, timu ya JKT ikiongozwa na meneja wao Ngowi ilifika uwanjani mapema saa 12 za
jioni, masaa matatu kabla ya kuanza mchezo huo ulioanza 2 usiku.
Baada ya hapo wachezaji wa timu hiyo waliingia uwanjani wakifanya mazoezi madogo madogo wakisubiri mchezo kuanza, huku Outsiders ikifika uwanjani saa 1:30 usiku.
Katika mchezo huo, JKT, iliyoonekana imejipanga vizuri, iliweza kuongoza kwa pointi 21-9 katika robo ya kwanza, wakati ile ya pili Outsiders ikapata pointi 20-13 na hadi kufikia mapunziko washindi walikuwa wanaongoza kwa pointi 34-29.
Robo ya tatu JKT iliweza kuongoza tena kwa pointi 17-9 na robo ya nne ikaongeza tena pointi 19-17, huku Jonas Mushi alitamba katika mchezo huo kwa kufunga pointi 22 na upande wa Outsiders alikuwa Tyrone aliyefunga pointi 15.