Kwa usiku wa saba mfululizo maelfu ya raia wa Georgia ambao ni wafuasi wa Umoja wa Ulaya wanaandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Tbilisi wakiipinga serikali ya kitaifa ya kihafidhina. Wakati maandamano hayo yakiendelea nchini Georgia nchi jirani ya Ukraine imemuwekea vikwazo Waziri Mkuu wa Georgia Bidzina Ivanishvili, anayeonekana na wengi kama kiongozi mkuu wa nchi hiyo.
Waandamanaji nchini Georgia waliizingira mitaa na kuzifunga barabara katika mji mkuu wa Georgia wakitaka kuendelezwa kwa sera zinazounga mkono Umoja wa Ulaya katika nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa Jamhuri ya Kisovieti.
Soma zaidi. Maandamano yaendelea Georgia kwa siku ya saba mfululizo
Haya yote yanafanyika baada ya uamuzi wa chama tawala kinachoiunga mkono Urusi cha Georgian Dream kukamwisha mchakato wa nchi hiyo kujiunga katika Umoja wa Ulaya wiki kadhaa zilizopita.
Kila ikifika majira ya jioni katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo, Tbilisi vikosi vya polisi na vikosi vya kijeshi vimekuwa vikikusanyika katika viunga vya mji huo kukabiliana na waandamanaji ingawa hakuna hatua kali zilizochukuliwa kwa waandamanaji wanaojitokeza.
Hata hivyo, duru za ndani za nchi hiyo zinasema wanasiasa wengi wa upinzani wamekamatwa siku ya Jumatano.
Soma zaidi. Polisi nchini Georgia yawakamata waandamanaji 107 katika mji mkuu Tbilisi
Kupitia mtandao wa X, msemaji wa mkuu mpya wa sera ya nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alitoa ripoti iliyoelezea kuwepo kwa vitendo vya kukamatwa kiholela, vurugu, na unyanyasaji wa waandamanaji huko akizitolea mwito pande zote kutojihusisha na vurugu.
Hali hiyo inayoendelea nchini Georgia imesababisha kujiuzulu kwa baadhi ya wanadiplomasia na watumishi wengine wa umma, ikiwa ni pamoja na afisa mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, hayo ni kulingana na shirika la habari la Georgia Interpressnews.
Ukraine yaweka vikwazo kwa waziri mkuu wa Georgia
Katika hatua nyingine, Rais wa Ukraine Volodmir Zelensky amesema kupitia mtandao wa telegram kwamba serikali ya Georgia ni kama inajikabidhi kwa Urusi.
Zelenskyy ”Serikali ya sasa ya Georgia inaisukuma nchi kuelekea kwenye utegemezi wa wazi kwa Urusi. Ni aibu wanachofanya dhidi ya watu wao. Na wakati Moscow inaisifu serikali hii ya Georgia, inaonyesha wazi ni nani wanafanya kazi huko Tbilisi na nani wanatawanya maandamano, kwa hakika si kwa ajili ya Georgia.”
Kufuatia hatua hiyo, Ukraine imemuwekea vikwazo Waziri Mkuu wa Georgia na bilionea Bidzina Ivanishvili, anayeonekana na wengi kama kiongozi mkuu wa nchi hiyo.