Madai wanafunzi 14 kufukuzwa shule kisa Chadema, Mkenda asema…

Moshi. Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameagiza timu ya wataalamu udhibiti ubora kwenda kuchunguza taarifa ya wanafunzi 14 wa Shule ya Msingi Izinga, iliyopo Nkasi Kusini kufukuzwa shule kwa madai ya wazazi wao kuiunga mkono Chadema kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mapema leo Desemba 5, 2024 ilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza wanafunzi 14 wa shule hiyo kufukuzwa shule kwa madai ya wazazi wao kukiunga mkono chama hicho.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Profesa Mkenda amesema amesikitishwa na taarifa hiyo na kwamba tayari asubuhi hii ametuma jopo la wataalamu kwenda kuchunguza ukweli wa taarifa hiyo.

Amesema watoto wote wa Kitanzania wanayo haki ya kusoma na kwamba hakuna mwenye mamlaka ya kumtoa mtoto shuleni kwa sababu ya mrengo wa kisiasa wa wazazi au walezi wao.

“Nimeona taarifa za wanafunzi kwamba waliondolewa shule kwasababu wazazi wao ni wanachama wa Chadema, nimeshangazwa sana na taarifa hii na tayari timu yetu ya wadhibiti ubora nimeituma asubuhi hii ifike pale shuleni ituambie ukweli kuhusu jambo hili.

“Napenda nitoe msimamo wa Serikali kwamba watoto wote wa Kitanzania wana haki ya kusoma hakuna mwenye mamlaka ya kumtoa mtoto shuleni kwasababu kama hizo,” amesema Profesa Mkenda.

Profesa Mkenda amesema baada ya timu hiyo kwenda kuchunguza taarifa hizo asubuhi hii na kuujua ukweli wake hatua nyingine zitafuata.

“Natafuta ukweli tujue kwanza halafu tujue hatua itakayofuata, kila mtoto Mtanzania ana haki ya kusoma, hatubagui na hakuna sababu ya kumbagua mtoto kwa sababu ya mrengo wa kisiasa.

“Maelekezo ya Rais wetu (Rais Samia Suluhu Hassan) ni kwamba hata mabinti waliopata mimba wanarudishwa shuleni kusoma, sembuse tu kwamba mtu amejiunga na chama cha siasa,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema baada ya timu hiyo kufika shuleni hapo na kutoa ripoti Serikali itatoa taarifa rasmi na hatua ambazo zitachukuliwa.

“Tutapata ukweli asubuhi hii na timu yetu ya wadhibiti ubora imeelekea kule na itatoa ripoti na sisi tutatoa taarifa kwa umma na hatua ambazo tutachukua,” amesema Profesa Mkenda.

Related Posts