Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Mabondia maarufu wa ngumi za kulipwa nchini, Karim Mandonga na Dulla Mbabe wameahidi kuwapa raha mashabiki wa masubwi Tanzania hasa Kanda ya Ziwa wakati wa mapambano yao ya siku ya Boxing Day iliyopewa jina la ‘Tagi la Mama Samia’ Desemba 26,2024 yatakayofanyika Uwanja wa Zimbihile, Muleba mkoani Kagera.
Katika siku hiyo ambapo mabondia mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi watapanda ulingoni, ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa muonekano mpya wa kinywaji cha Smart Gin ambao ni wadhamini wa pambano hilo yatafanyika pia matukio tofauti tofauti ya burudani.
Kuelekea siku hiyo mabondia hao ni kama wamevurugwa wakitamani tarehe ifike haraka ili kudhihirisha ubabe wao kwa kuwapiga wapinzani wao kwa mara nyingine.Mandonga atachapana na Said Mbelwa, huku Dulla Mbabe akizipiga na mkongwe Mada Maugo.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 5,2024 jijini Dar es Salaam, Mandonga ametamba kuwa atampiga vibaya Mbelwa kuliko amara ya kwanza na safari hii atatumia ngumi aliyoipa jina la Kiberenge, huku Dulla Mbabe akijinadi na mtindo kivita.
Mandonga amesema “Nitaendelea kumpiga Said Mbelwa mimi ndio Mandonga Mtu Kazi akae akijua kipigo kinamhusu sisi ni jiko la shamba halichagui. Mara ya kwanza alishindwa kumaliza raundi na safari hii hatoboi raundi mbili pale Muleba kwa hii ngumi kiberenge,”
“Kifupi tu naweza kusema tunakwenda kwenye vita, yule Maugo anajiita Mbunge wa Rorya sasa nimwambie tu mimi ni Mbunge mtarajiwa wa Kisarawe. Pamoja na kwamba tunakaa wote Chanika siangalii hilo safari hii nitamkanda, mara ya kwanza alijipendekeza nikamvunja kiuno sasa tukutane tarehe 26 mtaona nitakachomfanya,” ametamba Dulla Mbabe.
Kwa upande wake Mratibu wa Matukio kutoka kwa wandaaji wa pambano, Bakari Khatibu amesema kwa mara ya tano wanakwenda kufanya kitu chenye ubora huku wakisherehekea uzinduzi wa muonekano mpya wa Smart Gin.
“Tumekuwa na bidhaa nyingi za Smart Gin lakini safari hii kumekuja na muonekano mwingine mpya wa Keni, hivyo katika kusheherekea uzinduzi wake tunaanza na tamasha la ngumi la kihistoria pale Muleba mkoani Kagera tukiwa pamoja na PeakTime ambao ni wadau wetu tupo nao kwa muda mrefu,” amesema.
Mabondia wengine watakaopanda ulingoni siku hiyo ni ,Anuary Mlawa na Amiry Matumla, Ayoub Mwankina dhidi ya Mkongo Man Reagan Pacho, Jamal Kunoga na Kharidi Karama, Osama Alabi na Adam Peter, Chidi benga wa Songea dhidi ya Badiru Komugemu na Hidaya Zahoro wa Morogoro dhidi ya Happy Daudi.