Marie Stopes yaeleza umuhimu wenye ulemavu kupata huduma za afya ya uzazi

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkazi wa Marie Stopes Tanzania, Patrick Kinemo amesema shirika hilo linatoa huduma za afya ya uzazi kwa wananchi wote ambao wanastahili na wanahakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma hiyo.

Amesema shirika hilo linaloshughulika hasa na huduma za afya hususani za uzazi linahakikisha watoa huduma wao wamepata mafunzo jinsi gani ya kuongeza ushiriki wa kundi hilo katika ngazi mbalimbali.

Ameyasema hayo leo Alhamisi, Desemba 5, 2024 wakati akichangia mada kwenye mjadala wa Mwananchi X-Space (zamani Twitter) ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Marie Stopes Tanzania na wadau wengine wa afya.

Mjadala huo unamada isemayo, “Nafasi ya watu wenye ulemavu katika kukuza ustawi wa upatikanaji huduma za kijamii, elimu, afya na fursa za kiuchumi.”

“Kwa mwaka 2023 tulihudumia watu wenye ulemavu kwa asilimia tano kati ya watu milioni moja na nusu, tunajitahidi kuhakikisha tunawafikia huku tukishirikiana na Serikali,” amebainisha Kinemo.

Awali, akichokoza mada, Mhariri wa Afya la Mwananchi, Herrieth Makwetta amesema watu wenye ulemavu wamekuwa wakikutana na matukio ya unyanyapaa katika jamii ikiwemo kukosa ajira licha ya kuwa na uwezo wa kufanya kazi.

Hilo ni moja ya jambo ambalo wanatamani likomeshwe kwani mara nyingi wamekuwa wakipata elimu lakini fursa za ajira zinakuwa kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na wale wasio na ulemavu.

Shirika la Afa Duniani (WHO) linaeleza kuwa ni takribani asilimia 28 ya watu wenye ulemavu ndiyo walioajiriwa kikamilifu.

Makwetta amesema katika kupambana na hali hiyo ni vyema jitihada zikaongezwa licha ya kuwapo kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwemo kuzindua Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi wa Watu Wenye Ualbino (MTHUWWU) na Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi, uliozinduliwa Desemba 3, 2024.

“Mpango huu unalenga kulinda utu, usawa, na ustawi wao kupitia nguzo za kukinga, kuzuia, usawa na uwajibikaji. Hivyo ni vyema kuimarisha utekelezaji wa sera na sheria, kuhamasisha jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu, kuwekeza zaidi katika miundombinu na teknolojia jumuishi,” amesema Makwetta.

Kwa upande wake, Msimamizi Programu ya EngenderHealth, Lilian Lukumai amesema utumiaji watu wenye ulemavu kuwahamasisha wenzao kuchangamkia fursa za kupata afya bora inasaidia kuwapata wenzao kwa wingi.

Amesema kwa mwaka 2023 shirika lake liliweza kuhudumia watu wenye ulemavu 22,000 katika mikoa minane wanayofanya kazi huku akiweka bayana hamasa waliyonayo katika kupata huduma ni kubwa lakini changamoto ni uelewa.

Uelewa huo unatokana na jamii inayowazunguka kutoona umuhimu wa watu wenye ulemavu wana fursa sawa za kupata huduma mbalimbali ikiwemo za afya na kijamii.

“Sisi kama Engenderhealth tunawasogeza karibu na katika kufanya hivi tunawatumia watoa huduma ngazi ya jamii, ambao kati yao ni makundi ya watu wenye ulemavu ili kuweza kuwahamasisha watu waliopo kwenye taasisi zao kuja katika hizi huduma,” amesema Lilian.

Amesema katika ufanyakazi kazi miongoni mwa changamoto walizobaini ni ugumu kwa watu wenye ulemavu kufikia vituo vya afya, watoa huduma wengi wa afya wanashindwa kuwasiliana na watu wenye ulemavu hasa viziwi, miundombinu isiyokuwa rafiki, vifaa na uelewa wa jamii kuwa mdogo kwani jamii inawatenga na kuona hawana haki.

Related Posts