Mifuko ya pamoja uwekezaji inavyofanya kazi, faida zake

Fikiria wewe na majirani zako mnataka kununua kipande cha ardhi kwa ajili ya kilimo, lakini hakuna mmoja wenu mwenye pesa za kutosha kufanya hivyo peke yake. Hivyo, mnaamua kuchangishana ili kununua shamba, mnaajiri mtaalamu wa kilimo kusimamia shamba, na baadaye, faida inayopatikana kutoka kwenye mauzo ya mavuno inagawanywa kulingana na kile kila mmoja alichochangia.

Mfano huuhuu tunaweza kuutumia kuonesha jinsi mifuko ya uwekezaji fedha ya pamoja inavyofanya kazi, na jinsi inavyoweza kuleta faida kwa wawekezaji.

Mifuko ya uwekezaji ya pamoja (Collective investment schemes (CIS)) ni mtindo wa kuwekeza, ambapo fedha za watu mbalimbali zinakusanywa na kuwekezwa katika masoko ya mitaji na biashara nyinginezo.

Kampuni zinazoundwa kwa ajili ya kusimamia mifuko hii huwa na wataalamu wa fani mbalimbali za kifedha, uwekezaji na biashara. Kampuni hizi zinahitaji mtaji ili kuweza kuwekeza katika biashara zinazofaa na zinazoweza kulipa faida nzuri. Hivyo, zinakusanya mitaji kutoka kwa watu mbalimbali ili kupata kiasi cha kuanzia kwa uwekezaji (pooling of funds).

Kwa namna nyingine, badala ya mtu mmoja kuwekeza peke yake kwa kununua hisa, hati fungani na mengineyo, wanachama (watu binafsi, mashirika, n.k.) wanachangia fedha zao kwenye mfuko wa pamoja, ambapo wataalamu wa kampuni husika hutumia uzoefu wao kuamua wapi na vipi fedha hizo zitumike ili kupata faida bora.

Kazi kuu ya kampuni inayosimamia mfuko wa uwekezaji ni kuhakikisha kwamba maeneo ya kuwekeza yanachaguliwa vyema, na kwamba fedha zilizokusanywa zinagawiwa kwa mchanganyiko wa aina mbalimbali za uwekezaji ili kuepuka hatari ya hasara inayoweza kutokea ikiwa fedha zote zitawekwa kwenye chombo kimoja.

Faida katika CIS zinatokana na vyanzo viwili vikuu. Kwanza, mapato yanayotokana na uwekezaji, mfano kama mfuko umewekeza kwenye hisa za makampuni, faida inaweza kupatikana kutoka kwenye gawio la hisa au riba kutoka kwenye dhamana.

Pili, faida inapatikana kwa kuuza uwekezaji kwa bei ya juu. Kwa mfano, mfuko unaweza kuwa umeinunua hisa wakati bei ilikuwa Sh500, na sasa bei imepanda hadi Sh550; kuuza hisa hizo kutaleta faida kutokana na ongezeko la bei.

Faida hizi zinagawanywa kwa watu walioweka mitaji, kulingana na mchango wao. Mfano, kama umechangia asilimia 10 ya mtaji wa mfuko, utapata asilimia 10% ya faida hiyo kwa kipindi fulani, na kwa njia nyingine, kwa kuzingatia kiasi ulichochangia na asilimia ya umiliki wako katika mfuko.

Kuna faida kadhaa za kiuwekezaji katika mifuko ya aina hii:

Kwanza, unaweza kupata fedha yako uliyowekeza kwa haraka. Ikiwa utapata dharura au kuona fursa mpya, unaweza kuuza umiliki wako na kurudisha mchango wako kulingana na taratibu za mfuko.

Pili, mifuko ya uwekezaji ya pamoja inafanya uwekezaji kuwa rahisi kwa watu wenye uwezo tofauti kifedha, siyo tu kwa matajiri. Kwa mfano, kwa kiasi kidogo cha shilingi 10,000 unaweza kuwekeza katika mifuko hiyo, kama vile UTT AMIS, na mifuko mingineyo.

Tatu, si kila mtu ana muda wa kufuatilia mwenendo wa soko la hisa au biashara fulani kwa undani, na pia inahitaji utaalamu wa fani fulani kuelewa biashara hiyo. Hata hivyo, mifuko ya uwekezaji ya pamoja inasimamia na kuendesha uwekezaji wako kwa niaba yako, kuchagua wapi pa kuwekeza, na kufuatilia mwenendo wa biashara.

Nne, uwekezaji unafanyika kwa kuwekeza katika maeneo mbalimbali, kama vile shamba lenye mazao tofauti. Ikiwa zao moja halitamea, jingine linaweza kufanikiwa. Hii inamaanisha kwamba mifuko ya uwekezaji huchanganya aina mbalimbali za uwekezaji ili kupunguza hatari ya hasara kubwa ikiwa moja ya uwekezaji hautaendelea vizuri (portfolio investment).

Hata hivyo, zipo changamoto. Ada zinazotozwa na wasimamizi wa mifuko zinaweza kupunguza sehemu ya gawio au faida ya mwekezaji. Pia, Watanzania wengi wanakutana na changamoto ya kukosa uelewa wa masuala ya kifedha, ikiwemo maarifa kuhusu jinsi mifuko hii inavyofanya kazi.

Kwa kumalizia, ikiwa wewe ni mwalimu, mkulima, au dereva wa bodaboda, mifuko ya pamoja ya uwekezaji inaweza kuwa njia yako ya ukuaji wa kifedha. Anza kidogo, kuwa na taarifa, na acha nguvu ya wengi ikufanyie kazi.

Related Posts