Karagwe. Mili ya watu sita kati ya saba waliofariki dunia kwa ajali iliyohusisha magari matatu katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera imetambuliwa na ndugu na kuagwa kwa ajili ya mazishi.
Ajali hiyo ilitokea Desemba 3, 2024 na kusababisha vifo vya watu saba na majeruhi tisa katika eneo la Kijiji cha Kihanga baada ya lori aina ya Scania lilokuwa limebeba mizigo (parachichi) kugonga magari mawili ya abiria Toyota Hiace na Coaster.
Miili hiyo imeagwa katika Kituo cha Afya Kayanga wilayani humo ilipokuwa imehifadhiwa huku mwili mmoja ukiwa bado hujatambuliwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Karagwe, Happiness Msanga ametaja majina ya watu watano kati ya saba waliyotambuliwa na kupoteza maisha kuwa ni Rumanyika Charles (25), Theresia Sebastian (64), Amanda Alferd (3), Milembe Ezironi mtoto (miezi 8), Matha Deo Msambi mwanamke (23).
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Julius Raizer amesema Serikali imechangia upatikanaji wa majeneza yote saba na pole ya Sh450,000 kwa kila famila, pia kati ya waliofariki dunia, watatu ni raia wa Uganda na mmoja wa Rwanda.