BAADA ya jana kupigwa michezo mitatu ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 64 bora, uhondo huo utaendelea tena kesho kwa mechi nyingine sita kuchezwa kwenye viwanja mbalimbali, kwa lengo la kusaka tiketi ya kutinga hatua ya 32 bora.
Katika michezo za kesho, itashuhudia timu mbili za Ligi Kuu Bara zikianza kampeni ya michuano hiyo ambapo KenGold ambayo inaburuza mkiani itakuwa na kazi pevu ya kujiuliza mbele ya Mambali FC ya Tabora, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
‘Wauaji wa Kusini’ Namungo itakuwa kwenye Uwanja wa Majaliwa kuikaribisha Tanesco FC ya Kilimanjaro, huku timu nne pekee za Championship zikiwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha zinapenya hatua hiyo na kutinga raundi inayofuata ya mashindano hayo.
Cosmopolitan itakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani kucheza na Nyota Academy ya Arusha huku ‘Chama la Wana’, Stand United chini ya Kocha Meja Mstaafu, Abdul Mingange itaikaribisha Bon Bosco kutoka Iringa Uwanja wa Kambarage Shinyanga.
Kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, Polisi Tanzania itacheza na Bukombe Combine ya Geita huku African Sports ikicheza na Mabingwa wa Mkoa wa Singida, Town Stars katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kituo cha TFF Mnyanjani mjini Tanga.
Wakizungumzia michezo hiyo Kocha wa KenGold, Omary Kapilima alisema licha ya kiwango cha timu hiyo kwa sasa ila mchezo huo watautumia ili kurejesha morali ya kikosi hicho, huku Mohamed Kijuso wa Cosmopolitan akiweka wazi wamejiandaa vyema.
“Tunacheza na timu ambayo kwa bahati mbaya hatuijui vizuri na hii ni kwa sababu hatujapata nafasi ya kuiona kama ambavyo wao wanatuona, ni mechi ya kuhakikisha angalau tunarudisha ile hali ya kujiamini iliyotoweka,” alisema Omary Kapilima.
Kwa upande wa Kijuso wa Cosmopolitan alisema wamejiandaa vyema katika mchezo huo na licha ya kutokuwa na matokeo mazuri kwa siku za hivi karibuni, ila amewataka nyota wa timu hiyo kutobweteka na kutumia faida ya kucheza uwanja wa nyumbani.