Mwaka 2024 ulikuwa wa kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, jambo ambalo linatajwa kuwa na faida kiuchumi kutokana na kutanua wigo wa uzalishaji bidhaa kwa ajili ya masoko ya nje, kutengeneza fursa za ajira na kuongeza mapato ya Serikali.
Uwekezaji huu wa mitaji pia ulikuja na fursa mbalimbali ya uzalishaji kupitia sekta ya kilimo, viwanda, biashara na usafirishaji.
Nguvu hizi hazikuelekezwa katika kupata miradi mipya pekee, bali kupanua uwekezaji na kuboresha ile inayoendeshwa na Serikali ambapo sekta binafsi ilikaribishwa kuchangamkia fursa mbalimbali za ubia katika miradi inayoendelea.
Mathalani Novemba mwaka huu Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kilieleza kuwa kinachakata miradi 84 iliyopo hatua mbalimbali tangu kilipoanza utekelezaji wa sheria namba 103 Aprili, 2024, kwa lengo la kuwa na mikataba yenye thamani kwa miradi husika.
Miradi hii ni tofauti na ile 800 iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) hadi kufikia Novemba, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Novemba 11, 2024 na kamishna wa kituo hicho, David Kafulila miongoni mwa miradi iliyosajiliwa, mradi pekee uliofikia hatua ya uwekezaji ni wa Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC).
Kafulila anasema chini ya mpango wa PPP, wanahitajika kuhamasisha mtaji wa binafsi wa Dola bilioni 9 (Sh23.7 trilioni) ili kuwezesha baadhi ya miradi ya ujenzi kuanza.
“Miradi chini ya PPP ipo katika hatua mbalimbali, baadhi ziko kwenye makubaliano, uchunguzi wa kina, tathmini, ununuzi na maelezo ya dhana. Ujenzi wa barabara ya Kibaha hadi Chalinze yenye thamani ya Dola milioni 340 na ujenzi wa barabara za mzunguko zenye thamani ya Dola bilioni moja uko katika hatua nzuri,” anasema.
Tofauti na kilichosemwa na Kafulila, mwaka 2024 pia ulikuwa wa kufanya mageuzi katika sekta ya usafirishaji, hasa katika upande wa reli baada ya Serikali kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya huduma, ikiwemo katika treni ya kisasa (SGR).
Baada ya kuitwa kuchangamkia fursa kwenye SGR, Kampuni sita za Kitanzania tayari zilionyesha nia, ikiwemo GSM, Bakhresa Group, Mohammed Enterprises Company Limited, Lake Oil, Azania na Jambo.
Mbali na SGR, pia Machi 20, 2024, ilishuhudiwa kampuni binafsi ya Bravo ikiingia makubaliano na Tazara yanayohusisha kuingiza treni mbili za mizigo zenye mabehewa 20 kila moja na kila behewa litakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani 50 (sawa na malori mawili).
Kufuatia kukaribisha uwekezaji huu wa mashirikiano na sekta binafsi, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi anasema jambo hilo litasaidia kusukuma maendeleo mbele kwa haraka.
Hiyo ni kwa sababu sekta binafsi haina ukomo wa kupata mitaji na inao uwanja mpana wa kupata fedha, hivyo kukiwa na fursa inayolipa mtaji utapatikana.
“Sehemu hii ikiwa na utaratibu mzuri ina nafasi nzuri sana ya kuchangia katika uboreshaji wa miundombinu,” anasema Dk Olomi.
Anasema kama nchi bado haijapiga hatua katika eneo hilo, kwa sababu ule moyo wa kukaribisha PPP haupo kutokana na kutokuwapo utayari.
Pia uwepo wa sera inayotekelezwa kikamilifu ni changamoto, jambo ambalo linaenda sambamba na utayari wa kisiasa.
“Kukiwa na mazingira ambayo hakuna utayari wa kisera, kisiasa na Watanzania, mtu yeyote anayetaka kuwekeza kwa ukubwa anakuwa anashindwa, ili mtu awekeze lazima ajiulize kama sera hiyo inakuwa na mwendelezo, isije kuwa mabadiliko ya kiuongozi yanapofanyika na jambo hili linabadilika,” anasema Dk Olomi.
Ili kupata matokeo zaidi katika upande wa PPP, anashauri kuwapo kwa utawala bora, kukomesha vitendo vya rushwa, kwani ili uwekezaji wa aina hiyo uwepo lazima utaratibu utakaotumika uwe umenyooka na isipokuwa hivyo hata mwekezaji ataona kuna hatari ya kutorejesha mtaji wake.
“Kama mwekezaji anakuja kwenye nchi yako anakutana na mazingira yenye vitu vinavyoweza kuchangia kurudisha nyuma hawezi kuwekeza, utawala bora unaokuja na uwazi ni jambo muhimu sana katika uwekezaji wowote,” anasema Dk Olomi.
Japokuwa PPP inatajwa kuwa na manufaa katika kuchochea ukuaji wa uchumi, Mchambuzi wa Biashara, Dk Balozi Morwa anasema ni vyema Serikali ihakikishe inafanya tathmini na kujua ni miradi gani inapaswa kuwekezwa kwa ubia wa sekta binafsi na wao.
Hiyo ni kwa sababu, baadhi ya miradi inapaswa kufanywa na serikali pekee na si kwa ubia na Serikali.
Hiyo ni kwa sababu umiliki wa sekta binafsi kwa kiasi kikubwa katika miradi mingine inaweza kufanya wananchi kupata huduma kwa gharama kubwa, jambo ambalo linaweza kuwafanya wananchi kuendelea kuwa maskini.
“Hii mara nyingi inaweza kuwa na manufaa kwa nchi ambazo zimeendelea, lakini huku kwetu sekta binafsi akiwa mmiliki wa hisa nyingi na akiachwa aendeshe huo mradi peke yake anaweza kuwa anapata hela nyingi lakini anaidanganya Serikali,” amesema Dk Morwa.
Mwaka huu pia unaweza kuwa ule ambao utaifanya Tanzania kuvunja rekodi ya kusajili miradi mingi ya uwekezaji iliyodumu kwa miaka 11.
Hiyo ni baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC), Gilead Teri kuweka bayana kuwa hadi Novemba 29, 2024 TIC ilikuwa imesajili jumla ya miradi 800, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni, lakini pungufu ya rekodi iliyowekwa mwaka 2013 ambapo kituo kilisajili miradi 865.
“Mwaka huu utakuwa mwaka wa rekodi, tangu mwaka 1997 tulipoanza kusajili rasmi miradi, mwaka 2013 ndio unaoshikilia rekodi, lakini sasa kuna uwezekano mkubwa wa kuivunja kutokana na ongezeko kubwa la miradi mwaka huu,” anasema Teri.
Teri aliongeza kuwa jambo zuri ni zaidi ni kuwa kati ya miradi iliyokuwa imesajiliwa hadi Novemba 29, 260 ni ya wazawa na zaidi ya nusu ya miradi yote ina ushiriki wa wazawa.
Teri anasema katika miradi iliyosajiliwa mingi ni ya uzalishaji wa bidhaa za mahitaji ya kila siku, sekta ya ujenzi, majengo, uchukuzi, kilimo na utalii.
Anasema mafanikio hayo ni matokeo ya mageuzi yaliyofanywa katika kuvutia uwekezaji kwa kubadilisha mazingira, huku akisema kuwa yako thabiti na yanavutia kuliko wakati wowote ule katika nchi.
“Mbali na mazingira ya kisera yanayovutia, pia Tanzania ina rasilimali nyingi, nishati ya uhakika, soko kubwa na nguvu kazi ya kutosha kufanya uzalishaji wenye tija na kumfanya kupata faida,” anasema.
Miradi iliyosajiliwa hadi Novemba mwaka huu ni asilimia 58 zaidi ya miradi yote iliyosajiliwa mwaka 2023.
Katika mwaka 2023, TIC ilifanikiwa kusajili miradi 504 ambayo ilikuwa na thamani ya Sh14.06 trilioni ambayo ilitarajia kuzalisha ajira zaidi ya 23,000. Thamani ya miradi hiyo ilikuwa ni ongezeko kutoka zaidi ya dola za Marekani bilioni 3 (zaidi ya Sh7.53 trilioni) iliyosajiliwa mwaka uliotangulia.
Katika ripoti ya robo ya pili ya mwaka iliyoishia Juni 2024 iliyotolewa na TIC, Russia ndiyo nchi iliyokuwa ikiongoza kwa kuleta mtaji mkubwa, ikiwa ni zaidi ya Sh886.48 bilioni, ikifuatiwa na China iliyoonyesha nia ya kuwekeza Sh473.28 bilioni.
Ulaya ilishika namba tatu kwa kuonyesha nia ya kuwekeza Sh438.05 bilioni, Bermuda Sh137.34 bilioni na Nchi za Jumuiya za Kiarabu zikiwekeza Sh98.8 bilioni.
Fedha hizi na nyingine zilizowekezwa kutoka nchi tofauti ziliwekezwa katika maeneo 12 ambayo ni kilimo, majengo ya biashara, miundombinu ya kiuchumi, nishati, taasisi za kifedha, rasilimali watu, viwanda, mafuta na madini, huduma, mawasiliano, utalii na usafirishaji.
Katika miradi hiyo, viwanda ndivyo viliongoza kwa kupata miradi 92, vikifuatiwa na sekta ujenzi wa majengo ya biashara yaliyokuwa 28, usafirishaji 22, utalii 21, kilimo miradi 11, huduma na nishati zikiwa na miradi mitano kila moja.
Hata hivyo, wakati kilimo kikiwa na miradi michache, lakini ndicho kinaongoza kwa kutengeneza fursa nyingi za ajira zinazotarajiwa kutolewa ambazo ni 76,023, huku sekta ya viwanda inayoongoza kwa kuwa na miradi mingi ikitarajiwa kuzalisha ajira 12, 667.
Wakati kuvutia wawekezaji ikiwa ni moja ya kinachofanyika, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Yohanna Lawi anasema kutangaza ni eneo dogo hivyo ni vyema kuhakikisha Serikali inaangalia namna ya kushusha gharama za uwekezaji, kuendeleza utulivu wa kisiasa, kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa.
“Juhudi zipo na zinaonekana, kama ujenzi wa treni ya kisasa (SGR), viwanja vya ndege vinajengwa, lakini haya yote ni vyema yaende sambamba na uwepo wa sera zinazotabirika kwa sababu hivi ndivyo vitu vinavyoweza kuvuta wawekezaji,” anasema Dk Lawi.
Anasema uwepo wa nishati ya uhakika nalo ni jambo linalopaswa kuzingatiwa, hasa kwa kuangalia njia mbadala zinazoweza kutumika kuzalisha umeme kama jua, upepo, joto ardhi.
“Kwa kadiri tutakavyoweza kusimamia na kuhakikisha hivi vitu vinapatikana ndivyo tutaweza kuvutia wawekezaji kutoka nje.