Katikati ya mpango wa Serikali wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, wananchi nao wamekuwa na bunifu nyingi za kuwawezesha watu kumudu mabadiliko ya tabianchi kwa namna tofauti.
Frank Msigwa ni mbunifu wa bidhaa mbalimbali, yakiwemo majiko yanayotumia nishati safi, ambaye anafanyia shughuli zake jijini Dodoma.
Mbunifu huyo anayeishi katika Kata ya Nala, karibu kilomita 15 kutoka katikati ya jiji la Dodoma anaeleza nini kilimsukuma kuingia katika ubunifu, alipozungumza na Mwananchi katika mahojiano
JIBU: Siku moja nilitoka shuleni nikakuta ndugu zangu wakubwa na mama hawapo nyumbani na kwa kuwa nilikuwa na njaa niliingia jikoni kusonga ugali.
Kwa bahati mbaya ugali haukuiva nikautupa jalalani. Suala hilo lilimkasirisha mama, alivyorejea nyumbani alinichapa sana kwa kuharibu unga.
Hali hiyo iliendelea kunikera, nikawa natafakari kila mara kuangalia ni jinsi gani naweza kupata mashine ya kusonga ugali bila kutegemea mtu.
Novemba, mwaka 2016 nilikiwa nilimaliza kidato cha nne, niliamua kujikita kwenye kubuni mashine itakayotatua changamoto hiyo, hasa nikilenga kwenye maeneo yenye watu wengi kama shule na taasisi za elimu.
Niligundua mashine ya kusonga ugali ambayo inatumia umeme wa jua katika kuzungusha mitambo ya kupikia huku gesi ndio ikitoa moto unaotumika kupika ugali.
Mashine ilikuwa na sehemu ya kuweka unga na sufuria, ambapo ukiwasha gesi, mashine inatambua kuwa maji yamechemka, ina mota zinazoruhusu unga utoke na mwiko uanze kusonga ugali. Ukishaiva, mwiko unaweza kupakua wenyewe na kuweka kwenye sahani.
Baada ya ugunduzi huo nilikwenda katika ofisi za Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kuwaeleza na kuwaonyesha.
Lakini safari ya ubunifu huo haikuzaa matunda, baada ya kupelekwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) kwa ajili ya kuchora mchoro wa ubunifu ambako pia haukukubalika COSTECH kwa maelezo kuwa unapaswa kutumia chanzo kimoja cha nishati.
Swali: Wazo la kuanza kubuni majiko lilitokana na nini
Jibu: Ubunifu huu nilianza mwaka 2022, baada ya Serikali kusisitiza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania na kwamba ifikapo mwaka 2030, asilimia 80 wawe wanatumia nishati hii.
Kila nikipita mtaani na kuona mama ntilie na baba ntilie wakitumia mkaa kupika na kupika vitumbua na nyama napata shauku ya kubuni kitu kitakachowasaidia kuondokana na nishati ya kupikia, ndipo nilipoamua kubuni majiko yatakayoleta suluhisho kwao.
Katika kipindi hiki cha miaka miwili na nusu, sikuweza kuzalisha kwa sababu akili na muda wangu niliuelekeza katika ubunifu wa kutengeneza majiko yatakayowasaidia wakinamama ntilie na baba ntilie kuchoma nyama, kupika vitumbua na wali kwa kutumia nishati safi.
Majiko haya ni tofauti kulingana na kazi yake, nimehakikisha moto unawaka mahali unapotakiwa tu na si kwingine ili kuepusha matumizi makubwa ya gesi wakati mtu anapotumia.
Kwa mfano mtu anayechoma vitumbua moto unakwenda moja kwa moja katika eneo ambalo mpikaji ameweka unga na lile la kupikia wali hivyohivyo moto unawaka kuzunguka sufuria na katikati hakuna moto kuzuia kuungua wakati unapikwa.
Swali: Unalionaje soko la ubunifu wako?
Jibu: Soko naliona kuwa kubwa na kwa jinsi ninavyofanya tathmini ndogo ya kuzunguka kwa watu wanaojihusisha na kuchoma nyama ambao wengi walikuwa wakiniuliza kuhusu bei.
Bei ya kuyauza naweza kusema kama nikishapata mashine za kuyaboresha majiko haya kwa kuyaongeza thamani kwa kutumia vifaa vilivyo bora zaidi. Nina imani kama yakiboreshwa nitapata soko pia nje ya nchi.
Mtu anayetumia mtungi wa gesi wa kilo tano ambao gharama za kuujaza ni Sh24,000, anaweza kutumia kwa siku 20 ukilinganisha na mkaa ambapo anaweza kutumia kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000 kwa siku 10.
Pia faida nyingine ni nyama inaiva kwa muda mfupi wa dakika 15, mwonekano unakuwa mzuri na linaweza pia kutumika hata kwa eneo lenye upepo kwa kuwa limetengenezwa kwa mazingira hayo.
Usafi kwa anayepika unakuwa wa hali ya juu kwa kuwa hashiki mkaa wala majivu, hakuna unapolitumia.
Swali: Katika safari yoyote ya mafanikio hakuwezi kukosa changamoto, kwako ni zipi?
Jibu: Awali nilikuwa nikifanyia shughuli zangu Kisasa Sheli jijini Dodoma, lakini nililazimika kuondoka katika eneo hilo ambalo wateja walikuwa wameshanizoea baada ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuwaondoa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara.
Lakini baada ya kuondolewa katika eneo hilo, nilipata ufadhili wa fremu ya biashara katika eneo la Nala jijini Dodoma, baada ya mmoja ya wateja wangu kuvutiwa na kazi ya kumtengenezea geti la nyumba yake.