NHIF yalegeza masharti Toto Afya

Dodoma. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeondoa ulazima kwa shule na vyuo kusajili wanafunzi 100 katika mchakato wa kupatiwa bima ya afya, badala yake wanafunzi  watalazimika kuchangia Sh50,400 kuanzia Januari, 2025.

Hatua hiyo imetangazwa ikiwa ni mwaka mmoja na miezi tisa tangu Machi 13, 2023 NHIF ilipotangaza kuwa watoto ambao awali walikuwa wakisajiliwa kupitia utaratibu wa bima ya afya ya ‘Toto Afya, watasajiliwa kupitia vifurushi vya bima ya afya au shule wanazosoma.

Taarifa ilieleza NHIF inafanya maboresho ya usajili na huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa Bima ya Afya ya ‘Toto Afya’.

Akizungumza leo Alhamisi, Desemba 5, 2024 kuhusu maboresho yaliyofanywa na NHIF, Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Dk Irene Isaka amesema katika kuongeza kasi ya usajili wa wanafunzi na watoto wenye umri chini ya miaka 21, mfuko umeunganisha mfumo wa usajili wa mfuko na taasisi zinazosimamia sekta ya elimu.

Taasisi hizo ni Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet) na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ili kurahisisha utambuzi wa wanafunzi na utoaji wa namba za malipo kwa wazazi au shule kutegemeana na chaguo la shule au chuo husika.

Amesema maboresho yameondoa ulazima wa shule au chuo kusajili wanafunzi 100 au zaidi, badala yake wanafunzi watajiunga  kwa idadi iliyopo.

“Tunawahamasisha wazazi kuanzia Januari mtoto anapofungua shule afike na Sh50,400 anasajiliwa na kuanza kupata huduma mara moja,” amesema.

Dk Isaka amesema hatua hiyo ni katika kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Akizungumzia maboresho ya mfumo huo wa usajili, Kaimu Mkurugenzi wa Wanachama, Hipoliti Lello, amesema kwa sasa unawawezesha wazazi au walezi kupokea namba za malipo na kulipia moja kwa moja bila kupitia chuoni au shule husika.

“Niwaombe wazazi kutumia fursa hii kujiunga na mfuko,” amesema Lello.

Kuhusu idadi ya wanafunzi wanaonufaika kwa sasa, amesema hadi kufikia Novemba 26, 2024 wanafunzi 147,953 wa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo, wenye umri chini ya miaka 21 wananufaika na huduma za mfuko.

Kuhusu utaratibu kwa watoto walio nje ya mfumo wa shule, Lello amesema:

“Utaratibu lazima aje (ajiunge) na mzazi au mlezi, anakuwa mtegemezi wake. Kama mzazi au mlezi si mtumishi atalazimika kuingia mlezi au mzazi na mtoto kupitia kifurushi kingine tofauti ambacho pia viwango ni tofauti.

“Hapa tulikuwa tunatafuta suluhu, tumelenga wale ambao wako shuleni, tumelenga huko kwa sasa kwa kuwa wataturudisha kule kwenye hasara.”

Lello amesema mfuko umeandikisha wategemezi 233,554 wenye umri chini ya miaka 21 kupitia wazazi na walezi wanaonufaika na huduma za mfuko kupitia mpango wa vifurushi, wafanyakazi wa sekta binafsi na umma.

Ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanajiunga, amesema mfuko unaendelea na kampeni maalumu ya uhamasishaji kwa wananchi kujiunga, wakiwamo wanafunzi kupitia shule.

Wakitoa maoni, wadau wa masuala ya afya na wazazi wamesema kurejeshwa kwa kifurushi hicho ni ombi la Watanzania wengi na kwamba, NHIF wanapaswa kuwa makini.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha watoa huduma za afya Tanzania (Aphtha), Dk Samwel Ogillo amesema suala hilo ni jema lakini akatoa angalizo.

“Sababu ya kuiondoa Toto Afya ilikuwa inafyonza mfuko pamoja na ile ya wazee wastaafu ilifanya mfuko ukawa unakufa, ikirejeshwa mfuko utaendelea kufa kama Serikali imechangia labda, sijui siwezi kutoa maoni kwa sasa mpaka niangalie usajili huo utakuwaje,” amesema.

Frederick Mollel, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, amesema watoto wake walikosa kwa muda mrefu bima kutokana na kufutwa kwa kifurushi cha ‘Toto Afya’ lakini kwa sasa anauona mwanga.

“Zamani nilikuwa nawakatia wote sababu wazazi siyo watumishi hatuna bima, tangu hapo ilikuwa vigumu kulipia matibabu kama mtoto ameumwa ghafla na sina fedha. Sasa watoto wangu wote wanne wanasoma mwingine yuko chuo, sekondari na shule za msingi. Nina uhakika wa matibabu baada ya kifurushi kurudi,” amesema.

Awali, Dk Isaka alitoa ufafanuzi kwa nini kifurushi cha Toto Afya kilifutwa, akieleza ni kutokana na hasara iliyokuwa ikitengenezwa.

Amesema tangu mwaka 2016/17 mpaka 2022/2023 fedha nyingi zilitumika.

Mwaka 2016/17 kifurushi kilichangia Sh633 milioni, lakini watoto walitumia Sh2.274 bilioni sawa na asilimia 359.

Amesema mwaka 2020/2021 kilichangia Sh5 bilioni lakini walitumia Sh46 bilioni na kuonyesha hasara katika mfuko.

“Mwaka 2023 pamoja na uhakiki na kuhakikisha watu hawatumii kadi ovyo, bado ilikuja kufikia asilimia 313 na hii imetokana na wengi waliojiunga kuwa tayari ni wagonjwa, akishaenda anatumia zaidi bima ya afya. Wengi wanasubiri mtoto mgonjwa au amepata ajali ndipo wanakata, ilileta hasara kwenye mfuko,” amesema.

Akizungumzia hali ya mfuko huo kwa sasa, Dk Isaka amesema katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kwa michango ya wanachama na mapato yatokanayo na uwekezaji na mengineyo, katika kipindi cha kuishia Juni 2024 ulikusanya mapato ya jumla ya Sh756.48 bilioni sawa na asilimia 101.3 ya lengo la kukusanya Sh746.76 bilioni.

“Kati ya kiasi hicho cha mapato asilimia 92 ni mapato kutoka michango ya wanachama, asilimia saba ni mapato yatokanayo na uwekezaji na asilimia moja ni kutoka mapato mengineyo,” amesema.

Dk Isaka amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Juni 2024, mfuko ulibaini madai yasiyo halali ya Sh5.44 bilioni kutoka kwa watoa huduma mbalimbali na kati ya hizo Sh2.59 bilioni zimerejeshwa, huku kadi 12,685 zilifungiwa.

Kuhusu hatua zilizochukuliwa, Dk Isaka amesema mikataba 11 ya watoa huduma imesitishwa hivyo kufanya jumla ya mikataba 55 kusitishwa tangu mwaka 2018.

“Watumishi watatu wa mfuko wamechukuliwa hatua za kinidhamu baada ya mashauri yao kukamilika na wengine wanane taratibu zinaendelea, hivyo kufanya jumla ya watumishi 11 kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

“Watumishi wa sekta ya afya wapatao 36 taarifa zao zimewasilishwa katika mamlaka zao za kinidhamu,” amesema.

Related Posts