BAADA ya mkongwe Kelvin Yondani kumalizana na Pamba Jiji sasa ni zamu ya Deus Kaseke ‘Mwaisa Mtu Mbadi’ ambaye pia amejiunga na timu hiyo tayari kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini humo.
Wawili hao wameshawahi kucheza pamoja na wanaungana na timu hiyo wakiwa wachezaji huru baada ya kila mmoja kutoka timu tofauti, Yondani akitokea Geita Gold iliyoshuka daraja, wakati Kaseke alikuwa anaitumikia Fountaine Gate (zamani Singida Fountain Gate).
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Pamba kimeliambia Mwanaspoti, kiungo huyo tayari ameungana na timu na anaendelea na mazoezi kujiweka tayari kwa ushindani mara baada ya dirisha dogo kufunguliwa na kuingizwa kwenye mfumo.
“Ni kweli tumemalizana na mchezaji huyo na tayari kaungana na timu kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kujiweka tayari na ligi, tunaamini uzoefu wake utaongeza chachu kikosini,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Timu yetu haina wazoefu wengi na imeanza vibaya msimu, hivyo tunaongeza nguvu kwa kusajili wachezaji wenye uwezo na wazoefu na ligi ili mzunguko wa pili ukianza tupambane kubaki Ligi Kuu.”
Alisema bado wanaendelea kuboresha timu yao na kabla ya dirisha kufungwa watakuwa wamekamilisha na wana imani kubwa na mapendekezo waliyopewa na kocha kuwa yatakuwa chachu kikosini.
Pamba Jiji ambayo imepanda daraja msimu huu, imecheza mechi 13 imeshinda mbili, sare tano na vipigo sita ikikusanya pointi 11 zilizowaweka nafasi ya 12 kwenye msimamo kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi.
Mbali na Singida Fountain Gate, Kaseke amewahi kutamba na Mbeya City na Yanga kwa vipindi tofauti.