Rostam: Hakuna nchi duniani iliyojenga uchumi kwa kutumia wawekezaji wa nje

Mfanyabiashara na mwekezaji, Rostam Aziz amesema kuna umuhimu wa kuwakumbatia wawekezaji wa ndani katika utekelezaji wa miradi ya ndani ili kujenga uchumi wa nchi.

Rostam ameyasema hayo leo Alhamisi, Desemba 5, 2024 kwenye mjadala ulioandaliwa na Clouds Media Group unaoongelea namna Serikali imefanya uwezeshaji kwa wawekezaji wazawa. Amesema mwekezaji kutoka nje anachoangalia ni biashara na faida ya haraka kisha aangalie fursa iliyoko nchi nyingine.

“Mfanyabiashara kutoka nje akija anafanya shughuli iliyomleta kwa kutazama faida, anakuja na watu wake anaowaamini kuwapa ajira na faida atakayoipata atawekeza huko alikotoka au sehemu anayotaka kwenda kuwekeza,” amesema Rostam.

Ameshauri kwamba miradi mikubwa ya nchi kama ujenzi wa barabara, madaraja na miundombinu mbalimbali wapewe wazawa waitekeleze ili kuzungusha pesa ndani ya nchi ambapo biashara zitazaana.

Amesisitiza hakuna nchi dunani iliyojenga uchumi wake kwa kutegemea wawekezaji kutoka nje kwakuwa wawekezaji kutoka nje wanachoangalia ni masilahi yake hadi anakuja nchini lazima ahakikishe faida yake inakua kubwa na siku akimaliza anaondoka.

“Serikali ijiwekeze katika kupendelea wawekezaji wa ndani ndio wawe na matumizi makubwa wa pesa za Serikali za miradi kwasababu ikibaki nchini watanzania wengi watanufaika. Kodi zitalipwa biashara zitazunguka,” amesema Rostam.

Imeandaliwa na Sute Kamwelwe

Related Posts