Serikali yaeleza hatua iliyofikiwa ujenzi wa chuo cha Tehama

Dodoma. Serikali ya Tanzania imefikia makubaliano na Benki ya Korea (K-Exim Bank) kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha umahiri wa Tehama kitakachojengwa Nala jijini Dodoma.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa ameyasema hayo leo, Alhamisi Desemba 5, 2024 wakati akielezea kuhusu ujenzi wa chuo hicho.

Silaa amesema chuo hicho cha umahiri kitakuwa na kazi ya vijana wenye bunifu za Tehama ambao wamezipata vyuoni au nje ya mfumo rasmi kuboresha bunifu zao za Tehama kuwa bidhaa zitakazouzwa ndani na nje ya nchi.

Amesema ujenzi wa chuo hicho ni utekelezai wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliielekeza wizara kutengeneza mazingira ya kusaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya Tehama.

 “Tuna vyuo vingi vinavyofundisha vijana masuala ya Tehama kwenye ngazi mbalimbali, sasa kazi ya chuo hiki ni kuboresha na kuwasaidia vijana wenye bunifu ili ziwe bidhaa za Tehama zinazouzika ndani na nje ya nchi,” amesema.

Amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanza majadiliano baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu ili muda ukifika ukianza kianze ujenzi wake ambao utadumu kwa miaka miwili.

“Pindi kitakapoanza kujengwa ndani ya miaka mwili kitakamilika na kuanza kuona matunda ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan,”amesema Silaa.

Aidha, Silaa amesema Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inampango wa kujenga vituo nane vya ubunifu nchi nzima.

Amesema kwa kukamilika kwa chuo mahiri ya Tehama kutaifanya Tanzania kuchangamkia fursa zote za Tehama katika sekta ya teknolojia.

 Naye Nice Stephen amesema chuo hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza ubunifu na kuibua teknolojia mbalimbali nchini.

“Lakini watusaidie kwa kuweka kiasi kidogo cha ada, kitakapokamilika ili tulio wengi tuweze kunufaika na mafunzo,”amesema.

Related Posts