Dar es Salaam. Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) uliotakiwa kufanyika Septemba 2024 sasa utafanyika Desemba 18 na 19, 2024 huku ajenda kuu ikiwa ni uchaguzi wa viongozi wakuu.
Mchakato wa uchaguzi huo ulifanyika kwa wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo ya mwenyekiti wa chama hicho, walichukua na kurejesha fomu wakitaka kujaza nafasi hizo.
Hadi Septemba 2024, waliojitokeza kwa nafasi ya uenyekiti ni pamoja na mwanasiasa mkongwe Wilfred Lwakatare, Maftaha Nachuma (makamu mwenyekiti wa CUF-bara), Jafar Mneke, Hamad Mohamed na Profesa Ibrahim Lipumba ambaye inadaiwa alichukuliwa fomu hiyo.
Hata hivyo, bado haijajulikana kama mwenyekiti aliye madarakani, Profesa Lipumba atagombea tena nafasi hiyo kuendelea kukiongoza chama hicho.
Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Septemba 13, 2024, lakini kutokana na changamoto za maandalizi na kupisha uchaguzi wa serikali za mitaa, ulisogezwa mbele hadi Desemba.
Uchaguzi huo utahusisha nafasi ya uenyekiti ambapo wagombea tisa wamejitokeza kuwania umakamu uenyekiti Tanzania bara na Zanzibar na wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho, lililopo kisheria kwa mujibu wa katiba yao.
Leo Alhamisi Desemba 5, 2024 Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Yusuf Mbungiro ameliambia Mwananchi uchaguzi huo utafanyika Desemba 18 na 19, huku idadi ya wagombea uenyekiti ikiongezeka kutoka sita hadi tisa.
“Desemba 11 tutapitisha wagombea wote waliojitokeza kuwania uongozi, wapo wagombea wengi lakini kwa upande wa uenyekiti wapo karibu tisa. Tutaanza na vikao vya kamati ya utendaji kisha baraza kuu,” anasema Mbungiro.
Septemba 9, 2024 Mbungiro alisema walisogeza mbele uchaguzi huo, sambamba uchukuaji nha urejeshaji wa fomu uliokuwa ukamilike Agosti 25, lakini dirisha hilo lilifungwa Oktoba 30.
“Tumesogeza muda mbele na mkutano wetu mkuu wa kuchagua viongozi utafanyika Desemba 2024. Kwa hiyo, dirisha la kuchukua na kurejesha fomu bado liko wazi pamoja na kuendelea na chaguzi kwa baadhi ya wilaya za kichama ambazo hazikufanya,” amesema Mbungiro.
Mbungiro alisema sababu nyingine ya kupeleka mbele uchaguzi huo ni kutoa uhuru kwa wilaya 27 za kichama ambazo hazikufanya uchaguzi watekeleze jukumu hilo.
“Wilaya nyingi za kichama zilikuwa zimefanya uchaguzi, lakini zilizobakia ni 27 zinatakiwa zifanye, lakini kama hawatafanya kwa muda huo kwa sababu mbalimbali, basi tutaendelea na uchaguzi mkuu,” amesema.
Hali ilivyo Chadema Kanda Kaskazini, Kati
Wakati CUF wakitangaza kufanya uchaguzi mkuu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini na Kati wameanza kutoa fomu za kuwania uongozi kwa Kanda hizo.
Kanda za Kaskazini na Kati zenye mikoa Singida, Dodoma, Morogoro, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga limefunguliwa Desemba 3, litafungwa Desemba 9 saa 10 jioni.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Benson Kigaila nafasi zinazowaniwa ni pamoja mwenyekiti na mwenyekiti wa kanda na mhazini, pia mwenyekiti, makamu na katibu mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha).
Nafasi zingine ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu na mhazini wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) na mwenyekiti, makamu, katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha).
Katibu wa Chadema, Kanda ya Kati, Emmanuel Masonga ameliambia Mwananchi baadhi ya makada wameanza kuchukua fomu hizo, zinazopatikana mtandaoni.
“Ni mapema kusema nani nani amechukua fomu, kwa sababu mchakato unafanyika kwa mtandao, lakini wakati wa kurejesha tutajua,”amesema Masonga.
Aprili 2024, Mwananchi ilidokeza baadhi ya makada wanaowani uenyekiti kanda ya Kati wakiwemo David Jumbe, Devotha Minja, Imelda Malei na Ezekia Chisingila, wakati Kanda ya Kaskazani ni Pamoja Michael Kilawila anayetajwa kuchukua fomu hiyo.