Tukio la Wakili Lusako ‘kunusurika kutekwa’ laibua mjadala, Polisi yafafanua

Dar es Salaam. Jeshi Polisi nchini, linafanya uchunguzi wa kubaini kilichomfanya Wakili Alphonce Lusako, kukimbia na kujirekodi sauti aliyoituma kwenye mitandao ya kijamii, wakati askari waliokwenda ofisini kwake kumkamata Emmanuel Mweta.

Leo Alhamisi Desemba 5, 2024 asubuhi Lusako akiwa ofisini kwake Makumbusho wilayani Kinondoni alijirekodi sauti ‘voice note’ akisema “Jamani natekwa kuna watu wamekuja ofisini wanasema wao ni maafande, natekwa natekwa jamani naomba mnisaidie.”

Muda mfupi baada ya sauti kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, zikaanza kutolewa video za picha za CCTV zikiwaonyesha watu wawili waliovalia kiraia wanaodaiwa kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi wakiingia katika ofisi hiyo.

Watu hao walionekana wakielekea ndani ya nyumba ambako Wakili Lusako alikimbilia na kujificha. Askari hao walionekana kumtafuta pasipo kumwona na video zinaonesha askari hao akiwemo mwanamke wakiondoka.

Hatua hiyo iliibuka mijadala mbalimbali mitandaoni juu ya tukio hilo hasa ikizingatia katika siku za karibuni kuwekuwapo na matukio hayo ya utekaji na mauaji yanayofanywa na watu wasiofahamika.

Jioni ya leo Alhamisi, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime ametoa taarifa kwa umma akizungumzia tukio hilo huku akiambatanisha picha ya mnato inayowaonesha askari hao wakimkimbiza Lusako.

Katika taarifa hiyo, Misime amekiri askari wa jeshi hilo kufika eneo hilo kwa lengo la kumkamata mthumiwa Emmanuel Mweta, ambaye awali alikamatwa na baada ya kudhamini aliruka dhamana kwa muda mrefu.

“Leo Desemba 5 mlalamikiaji alitoa taarifa polisi kwamba amemuona mtuhumiwa huyo, ikabidi askari wawahi kumkamata.

Tunaendelea na uchunguzi kubaini kilimchofanywa anayetajwa kwa jina la Alphonce Lusako kukimbia kisha kujirekodi ‘voice note’ na kuirusha kwenye mitandao ya kijamii.

“Siyo yeye aliyekuwa akitafutwa na askari waliofika pale na kujitambulisha kwake na kumweleza wamefika kwa nia ya kumtafuta Emmanuel Mweta,” amesema Misime.

Related Posts