Uchaguzi TOC wafutwa, Mtaka, Tandau kurudishiwa fedha

UCHAGUZI Mku wa Kamati ya Olimpiki uliokuwa ufanyike Desemba 28, umefutwa rasmi na Serikali.

Mchakato wa uchaguzi huo ambao ulianza tangu mwezi uliopita nao umesitishwa na wagombea wote, kurejeshewa fedha zao za fomu.

Wagombea hao ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka aliyekuwa akichuana na Makamu wa Rais wa TOC anayemaliza muda wake, Henry Tandau, Nasra Mohammed na Michael Washa katika nafasi ya urais.

Rais wa TOC anayemaliza muda wake, Gulam Rashid amesema kufanyika kwa uchaguzi huo kutaamuliwa ba mkutano mkuu utakaofanyika Desemba 28 mjini Dodoma.

Kuhusu sababu ya kufutwa, Gulam amesema walipokea barua kutoka kwa kaimu msajili wa vyama vya michezo Desemba 2, yenye kumb. Na. AC, 50/246/01 “B/13 iliyoeleza kuufuta uchaguzi huo.

“Katika barua hiyo, kaimu msajili alidai mchakato wa uchaguzi ulianza kwa kutumia rasimi ya katiba ambayo ilikuwa haijapata ithibati ya msajili wa vyama na klabu za michezo,” amesema Gulam.

Anasema barua ya msajii ilieleza jambo hilo limeibua malalamiko miongoni na wanachama wa TOC.

“TOC pamoja na kutopokea rasmi malalamiko hayo kutoka kwa wanachama wetu, tumeridhia kuufuta.

“Tutalifikisha suala hili kwenye mkutano mkuu ili kupanga tarehe nyingine ya uchaguzi,” amesema.

Gulam amebainisha wale wote walioomba nafasi za uongozi wapeleke risiti halisi za malipo waliyofanya ili warudishiwe fedha zao.

Nafasi ya rais fomu ilikuwa Sh 500,000 na ile ya ujumbe fomu ilikuwa Sh 200,000.

Wagombea 27 walijitosa kuwania uongozi katika uchaguzi huo, wanne wakichuana kuwania urais, wawili nafasi ya makamu wa Rais na waliosalia walikuwa wakiwania nafasi 10 za ujumbe.

Kwa mujibu wa Gulam, tayari TOC imefanya taratibu za kimataifa na kitaifa kulingana na  katiba yao.

“Tumekwisha pata ithibati ya kitengo cha sheria cha Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), Msajili wa vyama na vilabu vya michezo Tanzania Bara na Msajili wa Vyama vya michezo Zanzibar,” amesema Gulam.

Related Posts