Uchaguzi wafanyabiashara Kariakoo uliopisha uokoaji jengo lililoporomoka wafanyika

Dar es Salaam. Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) jijini Dar es Salaam imefanya uchaguzi wa kuchagua viongozi wapya watakaoiongoza jumuiya hiyo kwa miaka mitatu ijayo.

Nafasi zinazogombewa katika jumuiya hiyo ni mwenyekiti yenye wagombea wanne ambao ni Abas Abdul, Martin Mbwana anayetetea kiti chake, Severini Mushi na Fedrick Lutindi.

Kwa upande wa makamu mwenyekiti wagombea ni wawili ambao ni Mfaume Fadhili Mfaume, Hendry Kanje, huku nafasi ya Katibu Mkuu ikiwa na wagombea wanne ambao ni Peter Mbilinyi, Ombeni Sefue Eloki, Frank Nduta na Renatus Mlelwa.

Katika nafasi ya Makamu Katibu wapo wawili ambao ni Thadei Beda na Donat Kibwana na kwa nafasi ya wajumbe wapo wagombea 19 huku wanaotakiwa ni 15.

Uchaguzi huo unafanyika leo Alhamisi, Desemba 5, 2024 katika Hoteli ya Lamada, Ilala, ni baada ya kuahirishwa kutoka Novemba 20, 2024 kutokana na tukio la kuporomoka kwa ghorofa mtaa wa Mchikichi Novemba 16, 2024 na kusababisha vifo vya watu 31 na majeruhi zaidi ya 86.

Akizungumza na Mwananchi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Kasim Mfaume amesema uongozi uliopita ulimaliza muda wake tangu Septemba 25, 2024 ambapo Halmashauri Kuu iliitisha mkutano kwa ajili ya kujadili uchaguzi huo.

“Hata hivyo, uchaguzi huu umechelewa kutokana na Halmashauri Kuu kuchelewa kuandaa kamati ya uchaguzi hadi pale ilipofikia makubaliano ya kufanyika kwa uchaguzi Novemba 20 mwaka huu,” amesema Mfaume.

Amesema mbali na uchelewaji wa halmashauri kuu pia wakati wagombea wakiwa kwenye kampeni na maandalizi ya uchaguzi tukio la kuporomoka kwa jengo la Mtaa wa Mchikichi lililodondoka Novemba 16 mwaka huu ikawa sababu nyingine ya kusogeza uchaguzi kuamuliwa kufanyika leo Desemba 5, 2024.

Sughuli ya uchaguzi ilianza saa 3 asubuhi kwa kuhakiki majina ya wapiga kura ili kuepuka kuingiza mamluki ambao si wafanyabiashara wa Karikaoo au si wanajumuiya hiyo na kufungwa rasmi saa 7 mchana.

Wakati shughuli hiyo ikiendelea Jeshi la Polisi pia lilikuwepo kuhakikisha hali ya usalama na uchaguzi unafanyika kwa amani.

Mbali na hilo lakini wagombea wanaotetea nafasi ya Mwenyekiti Martin Mbwana na Katibu wake, Frank Nduta hawakuonekana katika eneo lililofanyikia uchaguzi.

Hivyo, ulipofika muda wa kuhesabu kura alihitajika mtu ambaye atahesabu kura kwa wagombea hao, huku wakitakiwa kuwapigia simu kuwaeleza kuwa wanasimamia kura zao.

Endelea kufuatilia kujua matokeo ya uchaguzi huo.

Related Posts