Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Kariakoo wameutaka uongozi mpya kujenga umoja ili kuwasaidia wanapokutana na changamoto mbalimbali huku wakiwaonya kuacha tabia ya kupandisha mabega na au kujisahau kwani wapo kwenye nafasi hizo kwa ajili yao.
Uongozi mpya utakaoongoza Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK) kwa kipindi cha miaka mitatu umepatikana leo Alhamisi, Desemba 5, 2024 katika uchaguzi uliofanyikia Hoteli ya Lamada, Ilala jijini humo.
Katika uchaguzi huo, Severini Mushi amechaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kupata kura 229 kati ya kura 448. Mushi amewashinda washindani wake watatu akiwemo Martin Mbwana aliyekuwa anatetea nafasi hiyo kwa kupata kura 12.
Wengine ni Fedrick Lutindi aliyepata kura 160 na Abas Abdul akiambulia kura mbili. Kwa upande wa makamu mwenyekiti wagombea walikuwa wawili ambao
Mfaume Fadhili Mfaume ameibuka mshindi kwa kupata kura 251 huku Hendry Kanje akiibuka na kura 180.
Nafasi ya Katibu Mkuu ilikuwa na wagombea wanne, Renatus Mlelwa ameshinda kwa kupata kura 204 akifuatiwa na Peter Mbilinyi kwa kura 86, Ombeni Eloki kura 84 na Frank Nduta aliyekuwa akitetea nafasi hiyo akiambulia kura 30.
Katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu walikuwa wawili, Donat Kibwana akiibuka mshindi kwa kura 218 akifuatiwa na Thadei Beda aliyepata kura 186.
Mwananchi ambalo lilikuwapo eneo la uchaguzi limeshuhudia uchaguzi huo ukifanyika huku Mbwana aliyekuwa akitetea nafasi ya mwenyekiti na Nduta akitetea ukatibu mkuu kutowashuhudia kushiriki kwao licha ya kura zao kusimamiwa na wapambe wao.
Baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, wafanyabiashara wakapata wasaha wa kuzungumza na uongozi huo mpya ambao nao umezungumza kile wanachotarajia kwenda kukifanya.
Wafanyabiashara wamedai wamekuwa wakikutana na changamoto ambazo zilihitaji msaada lakini walikosa kutokana na uongozi uliopita haukuwa na umoja na mshikamano.
Hayo yamezungumzwa kutokana na matukio yaliyotokea likiwepo la mgomo wa wafanyabiashara uliotokea Juni, 2024 wakilalamikia kuhusu masuala ya kodi.
Ombeni Mbala, mfanyabiashara wa Kariakoo amesema uchaguzi huu umekuwa na mvuto kwa sababu wanahitaji mabadiliko na si kuwa na kikundi cha watu katika ufanyaji kazi.
“Kuna viongozi huwa wanajisahau na kujiona wao ni bora kuliko watu wanaowaongoza na matokeo yake hawasikilizi wafanyabiashara zaidi ya watu wachache haya yaliyotokea na kufurahiwa kwa matokeo si kwa bahati mbaya,” amesema Mbala.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Johnson Minja amesema kumekuwa na tabia ya viongozi kuvimba na kudharau viongozi wengine kwa sababu ya utofauti wa taasisi.
“Ilifikia hatua kiongozi wa Kariakoo anakuwa juu kuliko wa Taifa kwa sababu ya kutumika kauli ya Kariakoo chanzo cha kuzaliwa kwa taasisi nyingine ambayo ni ya mkoa wa Dar ea Salaam na Taifa, hivyo nyie viongozi wapya tunaomba hili lisiwe sehemu yenu,” amesema Minja.
Naye makamu mwenyekiti mstaafu, Yahaya Ali ametoa ushauri wa kuandaliwa kwa mkutano kama wafanyabiashara walivyohitaji kwani ni kilio chao cha kila siku na si kusubiri kutokee majanga.
“Mmewasikia wafanyabiashara wanataka mkutano, fanyieni kazi jambo hilo ili liweze kuwasaidia na hii itawaweka karibu na watu wenu na kutokuvimba mabega,” amesema Yahaya.
Amesema katika uongozi wao wamekutana na majanga makubwa mawili lakini la mgomo liliwafanya wasilale usingizi kutokana na ukubwa wa tatizo na wakati huo kukiwa na changamoto za uongozi.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Taifa, Hamis Livembe amesema sasa ni muda wa ushirikiano na mshikamano na kuachana na yaliotendeka katika uongozi mwingine kwani Serikali ina maswali mengi kuhusu Kariakoo.
“Kitu ambacho watu hawakijui ni kuhusu tunavyokutana na watu wa Serikali kila siku swali lao ni kuhusu Kariakoo na tunapambana mno kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa sasa tukafanye kazi,” amesema.
Akihitimisha mkutano huo baada ya watu wote kuzungumza, mwenyekiti mpya Mushi amesema atahakikisha anafanyakazi na wafanyabiashara wote bila kujali kipato chao na kutopandisha mabega kwasababu ya cheo chake.
“Nawaahidi kufanyakazi iliyotukuka na nitashirikiana na nyinyi bega kwa bega kuhakikisha tunafikisha jambo hili mbele,” amesema Mushi huku shangwe zikiibuka kutoka kwa washiriki wa mkutano huo.
Amesema atahakikisha yale yanayohusu Kariakoo atasimamia kwa umakini kama alivyotoa ahadi kwa wafanyabiashara na kwenye mamlaka nyingine atafanya nao kazi kwa ukaribu na kuziheshimu ambazo ni jumuiya za ngazi ya mkoa na Taifa.
Katika kuhakikisha anafanya alichoaahidi wakati wa kampeni kwa kuanzia ameunda kamati ya mabadiliko ya katiba iliyopo kwa ajili ya kuangalia upungufu uliopo yanafanyiwa kazi.
Mbali na hilo, kutokana na mamlaka aliyopewa amemteua Fedrick Lutindi kuwa mshauri wake ambaye jina lake litapelekwa katika Halmashauri Kuu ambayo itaamua.