Rombo. Baadhi ya wanawake katika vijiji vitatu vya Samanga, Kirongo juu na Sangasa, wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wameeleza tishio la nyani wilayani humo linavyowaogopesha kutembea peke yao bila waume zao wakihofia kudhuriwa na nyani hao.
Wamesema nyani hao ambao hutembea makundi kwa makundi nyakati za asubuhi na jioni, wamekuwa ni tishio kwao na kwamba wanapovamia maeneo yao na kuwafukuza huwakonyeza na wakati mwingine huwazunguka na kuwaweka kati hali ambayo ni hatari kwa usalama wao.
Pamoja na hofu hiyo, wamesema kwa zaidi ya miaka saba wameshindwa kuendeleza shughuli za kilimo kutokana na uharibifu unaofanywa na nyani hao ambao wamekuwa wakila mazao yao mashambani.
Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwaondoa nyani hao na kwamba kwa mara kadhaa wamekuwa wakiahidiwa na serikali kuwaondoa nyani hao jambo ambalo halijazaa matunda.
Mmoja wa wanachi wa Kijiji cha Samanga, Prediganda Shayo amesema nyani hao wamekuwa kero kubwa na kwamba wanapoingia kwenye makazi yao na kuwafukuza hawaondoki na badala yake nyani hao huwaita kwa kuwakonyeza.
“Yaani nyani wakija nyumbani kwako wakikukuta ni mwanamke hawaondoki hata ukipiga kelele kiasi gani hawaondoki tena wanakuangalia na kukukonyeza na wanakuzunguka na wanatengeneza kitu kama duara ili wakubane hapo katikati kama huna akili ya kukimbia wanaweza kukufanyia kitu kibaya,” amesema Prediganda.
Pamoja na mambo mengine amesema wanashindwa kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji kwa kuwa nyani hao huvamia kwenye mabanda ya kuku na mbuzi na kisha kuvunja na kula mifugo yao.
“Yaani imefika mahali hata ukiotesha kitu shambani huwezi kutoka nje ya eneo hilo maana ukirudi utakuta shamba ni jeupe. Tunateseka sana, hatuwezi kuvuna chochote tunaishi maisha ya shida. Kwa mfano sasahivi ni msimu wa kilimo hatusubutu kulima, kwasabau ya hawa nyani,” amesema mama huyo.
Pia, ameongeza“Wakati wa kilimo cha mahindi watu tunashindwa kulima kwasababu hawa nyani wanaopita shimo kwa shimo kuokota mhindi mmoja mmoja. Kwa mfano ukafanikiwa kuyalinda mpaka yakafikia hatua ya kubeba wanakuja wanavunja mahindi yote na hata viazi wanafukua.”
Mwanachi mwingine wa Kijiji cha Kirongo juu, Tarsila Marandu amesema hofu ya nyani imekuja ni kubwa kwao na kwamba imefika wakati mume wake akiondoka nyumbani yeye haweza kutoka akihofia uharibifu unaofanywa na nyani hao.
“Hawa nyani wanatutesa sana, imefika mahali sifugi kuku wala mbuzi kwasababu ukifuga wanakuja kubomoa banda na kuondoka na kuku wote yaani ni kilio tunalia ambacho hakina wenyewe,”amesema Tarsila
“Ndani hatuna chakula kabisa tunanunua chakula, tumebaki kama watu ambao hawana baba wala mama, sasahivi mtu hudhubutu kutokana kabisa, baba akishatoka mimi sidhubutu mkitoka wote mkirudi hutakuta chochote ulichokiacha ndani,” amesema
Tarsila Agusti Oisso, mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo, amesema imefika mahali mke wake anaogopa kwenda kukata majani ya mifugo peke yake mashambani akihofia kufanyiwa ukatili na wanyama hao.
“Kwa mfano kama leo hawa nyani wamekuja hadi barazani kwangu nikiwa bado hata sijaamka, juzi kati wamenivunjia vyoo vya nyumba wakijiangalia, kwa kweli hawa nyani wamekuja ni kero sana, kwa mfano hapa nyumbani mama huwezi kwenda kukata majani peke yake, maana akikutana nao wanamkonyeza, nyani wamekuwa ni tishio kabisa, zaidi ya miaka 7 watu hawalimi wala kuvuna,”amsema baba huyo
Akizungumzia tatizo la nyani hao, diwani wa kata ya Kirongo Samanga, Prisila Shayo amesema imefika mahali watu wamekata tamaa kuhusiana na wanyama hao ambao wamekuwa ni kero kwa wananchi na kwamba watu wamekuwa na hofu na wanashindwa kuendeleza shughuli za kiuchumi.
“Imefika mahali wananachi wameshindwa kuilewa serikali kwasababu wakati tunagombea tuliwaekeza wananchi tutashirikiana na serikali kuhakikisha tunawaondoa hawa nyani na kupelekwa kwenye hifadhi zao lakini mpaka sasa hatujafanikiwa chochote.
“Kuna vijiji vitatu ambavyo wananchi wameshindwa kulima wakihofia uharibifu wa nyani kama kijiji Cha Samanga, Sangasa na Kirongo juu ambapo vimepakana na bonde la mto mlembea ambapo ni eneo ambako nyani wanapanda na bonde kutoka msituni hadi kwenye maeno ya wananchi,”amesema diwani huyo
Amesema wananchi hao kwasasa wamebaki kama ombaomba kwa kuwa hana kipato chochote kile wanachotegemea kutokana na uharibifu wa wanyama hao.
“Hawa wananchi hawalimi wala hawafanyi chochote, hakuna mazao wanayoweza kulima katika hayo maeneo kwasababu kama ni ndizi nyani wanashambulia, mahindi yanafukuliwa kwenye mashimo hata matunda kama parachichi nyani wanakula,”amesema Prisila.
Alipotafutwa Ofisa Wanyamapori wa Wilaya hiyo, Ismail Walele amesema zoezi la kuwapunguza nyani hao kwenye makazi ya watu linaendelea na kwamba wiki ijayo ipo inakwenda wilayani humo kupambana na nyani hao.
“Ni kweli changamoto ipo, lakini tulishaanza utaratibu wa kuwapunguza na zoezi la kuwapunguza linaendelea na wiki ijayo kuna timu inakuja kuongeza nguvu ya kuwarejesha hawa wanyama hifadhini, wananchi wajiandae kulima na mambo yatakaa sawa,”amesema Walele.