Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Utetezi na Ujumuishwaji wa Watu Wenye Ulemavu Hospitali ya CCBRT, Fredrick Msigallah amesema watu wenye ulemavu wamekuwa wakionekana hawana uwezo wa kujamiiana dhana ambayo siyo sahihi jambo hilo limefanya wanyimwe huduma za afya za uzazi.
Msigallah ameyasema hayo leo Alhamisi Desemba 5, 2024 kwenye Mwananchi X Space, inayoandaliwa na Mwananchi Communications Limited kwa kushirikiana na Marie Stopes Tanzania ikijadili mada isemayo “Nafasi ya Watu wenye Ulemavu Katika Kukuza Ustawi wa Upatikanaji Huduma za Kijamii; Elimu, Afya na Fursa za Kiuchumi.
Msigallah amesema si kweli watu wenye ulemavu hawawezi kujamiiana huku akifafanua hata akiwa amelema viungo basi viungo vya uzazi vinafanya kazi vizuri kama walivyo wasiokuwa na ulemavu.
“Dhana hii imekuwa ikifanya watu kuona kwanini tuwapelekee huduma za afya ya uzazi watu ambao hawawezi kujamiiana kitu ambacho si kweli, ni kwamba wanaweza kujamiina kama watu wengine na wanahitaji huduma za afya na uzazi wa mpango kwa kiwango sawa na wasiokuwa na ulemavu,” amesema.
Jambo hilo limekuwa likifanya CCBRT kuendelea kuweka mkazo suala la ujumuishaji watu wenye ulemavu hasa kwenye huduma za afya ya uzazi.
Amesema pia jamii imekuwa ikiona wenye ulemavu kama waliolaaniwa na mkosi katika jamii jambo ambalo limefanya wasishirikishwe katika fursa mbalimbali ndani ya jamii.
“Linapokuja suala la afya ya uzazi wa mpango na anaangaliwa kama mtu aliyelaaniwa ni dhahiri kuwa atatengwa katika kupata huduma mbalimbali za afya za uzazi kwa sababu ataonekana ni mkosi na hastahili kupata huduma hiyo na hii si tu kwa jamii bali hata watoa huduma,” amesema.
Kutokuwa na maamuzi ya kuchagua mtu anayepaswa kuwa naye katika mahusiano imekuwa ni changamoto nyingine ambayo wanakutana nayo watu wenye ulemavu jambo ambalo linafanya wachaguliwe wenza na watu wa karibu wakiwemo wazazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulamevu Tanzania (Shivyawata), Mkoa wa Mbeya, Bahati Bukubilo amesema elimu ya afya ya uzazi kwa wenye ulemavu imesaidia jamii kuwajali kwa kuacha kutoa maneno ya fedheha kwa kundi hilo.
Amesema hapo zamani baadhi ya watu walikuwa wakiwatolea maneno yaliyokuwa yakiwakatisha tamaa kundi hilo katika suala zima la uzazi.
Aidha amesema kupitia mafunzo ya Marie Stopes kundi hilo limepata elimu ya afya ya uzazi pamoja na jamii kwa ujumla na sasa wanawake mkoani humo wamekuwa huru kujieleza pale wanapoenda vituo vya afya.
“Tunajaliwa hivi sasa baada ya watu kupata elimu kutoka Marie Stopes ukilinganisha na huko nyuma. Hata wale wakalimani hawakuwepo ilikuwa ngumu kupata huduma katika vituo vya afya,” amesema.
Ameshauri kwamba elimu iendeee hadi vijijini kwa watoa huduma ya afya ili kuwafikia zaidi.