Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemtaka Mshauri elekezi Dohwa Engineering kampuni ya Korea anayesimamia miradi mikubwa ya ujenzi wa mfumo ya Majitaka nchini Tanzania kufanya kazi kwa viwango, kumaliza kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha.
Waziri Aweso amesema hayo jana Jumatano, Desemba 4, 2024 akiwa Seoul, nchini Korea Kusini katika mazungumzo na Kampuni ya Dohwa ambaye ni Mshauri elekezi wa mradi wa ujenzi wa mfumo wa Majitaka Katika jiji la Dodoma wenye thamani ya Dola 70 milioni ambao utanifaisha kata 21 za katika Jiji la Dodoma.
Kikao hicho kimejikita pia kujadili mustakabali wa mradi wa ujenzi wa mtandao wa uondoaji na majitaka na ujenzi wa mtambo wa uchakataji majitaka katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam ikiwemo Buguruni, Ilala, Kariakoo, Mchikichini, Jangwani, Gerezani, Kisutu, Upanga, Kivukoni, Mizimuni eneo la Kinondoni.
Sambamba na hilo, mradi mwingine wa majitaka kwa Jiji la Dar es Salaam wa Mbezi Beach wenye gharama ya Dola milioni 70 ambao upo asilimia 62 ya utekelezaji.
Waziri huyo amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria na imejizatiti vilivyo kumaliza changamoto ya ukosefu wa miundombinu ya majitaka nchini Tanzania hususan ikishirikiana vyema na nchi ya Korea Kusini.
Waziri Aweso yuko Korea Kusini kwa mwaliko maalumu wa Benki ya Exim ya Korea na Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Korea (EDCF).
Ijumaa Desemba 6, 2024, anatarajia kukutana na Makamu wa Rais wa Benki hiyo ili kujenga ushirikiano zaidi baada ya uwekezaji wa Serikali ya Korea kusini katika miradi ya Maji Taka kwa Majiji ya Dar es Salaam, Dodoma na Manispaa ya Iringa.
Waziri Aweso alipokewa na mwenyeji wake, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura.
Akiwa Seoul Korea, ametembelea moja ya kampuni kubwa za teknolojia katika sekta ya maji ya nchini Korea ya Green Tech. Inc ambayo imefunga mfumo wa mita janja (Smart Water Managemant System) katika manispaa 43 nchini humo pamoja na nchi nyingine, ili kujionea teknolojia hiyo pamoja na kuona namna mfumo huo unavyofanya kazi.
Waziri Aweso amesema Mamlaka ya Maji ya Iringa (Iruwasa) imepanga kufunga mfumo janja wa kusimamia menejimenti ya usambazaji maji mjini Iringa. Mradi huo utawezesha kupunguza upotevu wa maji na kusimamia ubora na msukumo wa maji katika mfumo wote wa usambazaji kupitia mfumo maalumu wa mawasiliano.