Na Happiness Shayo – Dar es Salaam
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Ujerumani ukiongozwa na Mkurugenzi anayeshughulikia Masuala ya Kusini mwa Jangwa la Sahara na Sahel kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mhe. Christoph Retzlaff lengo ikiwa ni kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Ujerumani hususan uhifadhi wa mazingira asili na mienendo ya miradi mbalimbali inayohifadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Wizara ya Maendeleo BMZ.
Kikao hicho kimefanyika leo Desemba 05,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijni Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili kuhusu kushirikiana katika maeneo ya Urithi wa Utamaduni wa Kikoloni (colonial heritage), Makumbusho ya Taifa na ushirikiano baina ya nchi hizo katika bioanuai.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Chana aliipongeza Ujerumani kwa namna ambavyo imekuwa ikitoa ufadhili nkatika miradi mbalimbali ya katika Sekta ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania ambayo imepelekea kukua kwa Sekta hiyo ambapo kwa sasa inachangia asilimia 17 katika Pato la taifa na asilimia 25 kwa fedha za kigeni.
“Uwepo wa watalii nchini umeongeza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja nchini ikiwemo kuwawezesha wajasiriamali wadogo kuongeza vipato vyao madereva tax, wauzaji wa vyakula na watoaji wa huduma za malazi hunufaika.” Mhe. Chana amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi anayeshughulikia Masuala ya Kusini mwa Jangwa la Saharana Sahel kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Christoph Retzlaff alisema kuwa Tanzania ni mshirika muhimu wa Ujerumani na Ujerumani ina nia ya kujenga uhusiano katika maeneo mengi zaidi hasa katika bioanuai(biodiversity).
Kikao hicho kimehudhuriwa na Balozi was Shirikisho la Ujerumani Tanzania, Mhe. Thomas Terstegen Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Hassan Mwamweta, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Gerald Mbwafu, Afisa Mambo ya Nje II, kutoka Wizara ya Mambo ya Nje. , Lisa Kilua, Mkuu wa Ushirikiano, Bi. Julia Kronberg na Naibu Mkuu wa Ujumbe Bw.Manuel Müller,Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa Tanzania, Dkt. Noel Luoga na wawakilishi kutoka Bodi ya Utalii Tanzania.