Waziri Mkuu wa Ufaransa awasilisha barua ya kujiuzulu – DW – 05.12.2024

 Wabunge wa Ufaransa walipitisha usiku wa Jumatano kura ya kutokuwa na imani na serikali ya Waziri Mkuu Michel Barnier ambaye tayari amewasili katika ikulu ya Elysée kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwa  Rais Macron.

Serikali ya Waziri Mkuu Barnier iliyodumu kwa miezi mitatu tu, inakuwa miongoni mwa zile zilizokaa madarakani kwa muda mfupi zaidi tangu mwaka 1958 na inakuwa mara ya kwanza kwa serikali kuangushwa kwa kura ya kutokuwa na imani bungeni tangu mwaka 1962.

Wabunge kutoka vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na kushoto waliunga mkono kuondolewa kwa Barnier kwa wingi wa kura 331 wakati kura 288 tu zilizokuwa zikihitajika. Hatua hii inalitumbukiza taifa la Ufaransa katika mzozo mkubwa wa kisiasa unaotishia uwezo wa serikali kuendelea vyema na majukumu yake.

Barnier avutana na wabunge wa Ufaransa

Bunge la Ufaransa
Bunge la UfaransaPicha: Aurelien Morissard/Xinhua/dpa/picture alliance

Chanzo za mzozo huu wa kisiasa, ni mjadala wa bajeti ya mwakani ambapo wabunge walikataa muswada uliopendekezwa na waziri Mkuu  Michel Barnier wakisema ulikuwa ukibana mno matumizi hasa kwenye mfuko wa kitaifa wa misaada ya kijaamii. Lakini Barnier alikaidi na kusaini muswada huo kwa kutumia sheria inayompa mamlaka ya kufanya hivyo, kitendo kilichowakasirisha wabunge.

Mara baada ya uamuzi huo kutangazwa, Barnier aliyekuwa pia Bungeni alishukuru kupata fursa ya kuitumikia Ufaransa.

“Sasa mumefikia wakati huu wa ukweli. Hatimaye, mniruhusu niseme kuwa binafsi, ninahisi kuwa nimepata fursa ya heshima ya kuongoza kwa muda wa miezi mitatu, na bado niko Waziri Mkuu wa Wafaransa wote, na wakati wadhifa huu utafikia mwisho, labda hivi karibuni, naweza kusema kwamba hii itabaki kuwa fahari kwangu kuitumikia kwa dhati Ufaransa na Wafaransa ”alisema Barnier katika hotuba yake.

Upinzani wamnyooshea kidole Barnier

Kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha RN Bi Marine Le Pen
Kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha RN Bi Marine Le PenPicha: Aurelien Morissard/Xinhua/IMAGO

Wabunge wa upinzani waliopanda jukwaani bungeni hapo walimnyooshea kidole  Barnier wakisema wakulaumiwa kwa hali hii ni yeye mwenyewe aliyeshindwa kuwashawishi wabunge na kutilia maanani matakwa ya Wafaransa walio wengi. Baadhi ya wabunge wa upinzani walikwenda mbali zaidi na kumtaka hata Rais Macron ajiuzulu wakisema utawala wake wote umepoteza imani ya Wafaransa.

Soma pia: Serikali ya Barnier wa Ufaransa yaangushwa bungeni

Kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Rally Bi Marine Le Pen amesema kulikuwa hakuna namna nyingine ispokuwa uamuzi huu uliofikiwa.

“Ili kuwalinda watu wa Ufaransa, hakukuwa na suluhisho jingine zaidi ya hili. Sitoi wito wa kujiuzulu kwa Emmanuel Macron. Ninachokisema ni kwamba utafika wakati, tusipochukua mkondo wa kuwaheshimu wapiga kura na kuheshimu nguvu za kisiasa na za uchaguzi, basi ni wazi kwamba shinikizo kwa Rais Macron litazidi kuongezeka. Lakini yeye pekee ndiye atakayekuwa na uamuzi na neno la mwisho, ” alieleza Bi Le Pen.

Licha ya shinikizo hilo linalomkabili, muhula wa Macron utamalizika mwaka 2027 na hawezi kung´atuliwa madarakani ispokuwa ajiuzulu mwenyewe.

(Vyanzo: AP, AFP)

 

 

Related Posts