KABLA ya kupewa fursa ya kuifundisha Ken Gold FC, Omary Kapilima hakuwahi kuhudumu kama kocha mkuu wa timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kiufupi ni kwamba Ken Gold ndio timu ya kwanza kumfungulia Kapilima mlango wa fursa ya kupata uzoefu wa Ligi Kuu akiwa kama kocha baada ya kucheza kwa mafanikio alipokuwa mchezaji.
Kwa maana nyingine Kapilima na Ken Gold ni pande mbili ambazo hazina uzoefu wa kutosha wa ligi yetu, upande mmoja ukikosa uzoefu wa nafasi ya ukocha na mwingine wa kitimu kwa sababu huu ni msimu wa kwanza kwa timu hiyo ya mkoani Mbeya.
Haitokei kwa bahati mbaya kwamba timu ambayo inafanya vibaya kwenye ligi inaamua kumpa fursa kocha asiye na uzoefu mkubwa wa ligi kama ilivyofanya Ken Gold kwa Kapilima hivyo ni lazima zipo sababu za msingi kwa wao kuamua hivyo.
Uongozi wa Ken Gold bila shaka umefanya tathmini na utafiti wa kina wa nini kinachoikwamisha timu na ili wakitafutie suluhisho wanahitaji kocha aina ya Kapilima wakiamini ni mtu sahihi kwao.
Kapilima kwa sasa ana kazi kubwa mbili pale Ken Gold ambazo akifanikiwa kuzikamilisha vyema, atajijengea wasifu mzuri na heshima kubwa katika maisha ya ukocha hapa Tanzania jambo ambalo litamfanya ageuke lulu siku za usoni.
Kwanza ni kuiwezesha timu kupata matokeo mazuri ili iweze kusalia katika Ligi na kazi ya pili ni kuboresha na kukuza kiwango cha mchezaji mmojammoja wa timu hiyo ili iwe imara zaidi na kuweza kuhimili ushindani wa ligi kwa mechi zilizobaki.
Ni wazi kwamba katika dirisha dogo, Kapilima ataongezewa watu kikosini lakini kwa uwekezaji ambao Ken Gold imefanya haiwezi ikapata wachezaji wa daraja la juu hivyo wale watakaopatikana bado watahitajika kupigwa msasa ili waingie kwa haraka katika staili ya timu.
Kama Kapilima akifanikiwa katika kazi hizo mbili, hapana shaka ataliweka jina lake katika chati ya makocha lulu wazawa nchini lakini ikishindikana, atahitaji kutumia nguvu kubwa hapo baadaye kuziaminisha timu kuwa yeye ni bora.