ARWFA yapania makubwa soka la wanawake Arachuga

CHAMA Cha Soka la Wanawake Mkoa wa Arusha (ARWFA) linaendelea na mikakati ya kuhakikisha wanainyanyua tena mchezo huo kuanzia ngazi ya chini wakiamini itasaidia tena kupata timu ya Ligi Kuu.

Arusha imewahi kuwa timu mbili za Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), ambazo ni Tanzanite Queens iliyokuja kuuzwa Dodoma mwaka 2020 na kuwa Fountain Gate Queens pamoja na The Tiger Queens iliyoshuka hadi Ligi Daraja la Kwanza mwaka 2023, ilihali Lengo Queens iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza nayo ilishuka daraja na sasa iko ngazi ya mkoa.

Kwa sasa haina timu ya madaraja hayo hali ambayo inaifanya ARWFA kuanza upya kwa kuibua vipaji kuanzia chini kupitia bonanza ambalo wamekuwa wakifanya  kila mwezi wakati huo wakiamini itawalipa kwa miaka ya hivi karibuni.

Bonanza ilo ambalo lilianzishwa Oktoba mwaka huu na kushuhudiwa mwitikio mdogo wa timu shiriki, lakini kwa sasa limepata umaarufu mkubwa jijini hapa kwani katika Novemba ilishuhudiwa timu zaidi ya 10 zikishiriki, nyingi zikiwa ni kutoka katika vituo vya kukuza na kulea vipaji vya soka kwa vijana.

Yasinta Amos ni Katibu wa ARWFA, ameiambia Mwanaspoti, mikakati yao ni kwamba katika kipindi cha miaka minne ijayo basi Arusha iwe ni miongoni mwa mikoa yenye timu za WPL, uwe ni mkoa ambao mawakala na timu zitakuwa zinatolea macho kuja kufanya usajili na kuchagua vipaji.

“Wakati tunaanza ilikuwa na ugumu lakini kwa sasa mwitikio umekuwa mkubwa sana hivyo timu nyingi zimekuwa zikihamasika kushiriki,” amesema Amos.

Ameongeza licha ya changamoto ya udhamini, lakini wapo baadhi ya wadau kama kampuni ya Bonite kupitia kinywaji cha Coca Cola na chama ha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA),zimekuwa zikishirikiana nao na kuongeza nguvu pale wanapokuwa wamekwama.

Zakayo Mjema, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), amesema mpango kazi yao kwa sasa ni kuwekeza katika soka la wanawake ambapo kwa sasa mwitikio na ushindani umeongezeka na vipaji vimezidi kuongezeka.

“Wazazi wamehamasika sana ndio maana unaona kuna timu za vijana wa umri kuanzia chini ya miara 9 na kuendelea tofauti na zamani mzazi alikuwa hawezi kuruhusu mtoto wa umri huo kuja kucheza asubuhi hadi jioni,” amesema Mjema, huku kwa upande wa Daudi Peter, Mkurugenzi wa Ufundi wa Black Eagle Sports Academy amesema bonanza ilo limekuwa likiwafanya wachezaji wao kujihisi kama wanashiriki mashindano makubwa lakini pia ni njia ya kuona kile ambacho wanakifundisha kinafanyiwa kazi kwa namna gani.

Bonanza hilo la kusaka vipaji ya ARWFA linashirikisha timu za kuanzia umri wa chini ya umri wa miaka kati ya 9 na 18 lengo kubwa ikiwa ni kuibua vipaji na kuhamashisha soka la wanawake mkoani humo.

Related Posts