DC Mwanziva:  Kina baba pelekeni watoto wapate chanjo

Lindi. Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva amewataka wanaume kujitokeza kuwapeleka watoto kliniki ili matone ya vitamini A na dawa za minyoo, badala ya kuwaachia wanawake jukumu hilo.

Utoaji wa huduma hiyo ulioanza Desemba mosi na utaendelea hadi Desemba 30 mwaka huu, umelenga kuwafikia watoto 20,668 katika Manispaa ya Lindi.

Akizindua kampeni hiyo ya utoaji wa matone hayo leo Desemba 6, katika kliniki ya mama na mtoto, Mwanziva amesema jukumu la malezi si la wanawake peke yao bali ni jukumu la wote.

“Kina baba nanyi mbebe jukumu la malezi, sio jukumu la kina mama pekee. Sio vibaya baba nawe ukibeba mtoto mgongoni na kumbembeleza na hata kuleta mtoto kliniki,” amesema, huku akiwapongeza wanaume waliopeleka watoto wao kupata chanjo.

“Ujumbe huu ufike hata kwa viongozi wa dini, makundi ya wafanya mazoezi hadi sokoni, huko ndiko kina mama wanakwenda kuhemea,” amesema.

Mwanziva amewataka wataalamu wa afya kupambana kusambaza kampeni hiyo kama wanavyopambania miradi mingine ya maendeleo.

Akitoa ujumbe kwa wanawake, amesema:  “Nanyi kina mama mliopo hapa mwende kuwa mabalozi kwa akina mama wengine amabao hawajafika hapa kuwafikishia ujumbe huu,” amesema.

Kuhusu mpango hupo, Ofisa Lishe wa Manispaa ya Lindi, Bakari Abdallah amesema wanatarajia kuwapatia matone ya vitamini kwa watoto zaidi ya 20,000 kwa kipindi cha mwezi mmoja.

“Tumezindua mwezi wa lishe kwa watoto chini ya miaka mitano kuanzia Desemba mosi hadi hadi 30. Lengo ni kuwafikia watoto kuanzia miezi sita hadi 59 (miaka mitano),” amesema.

Swalehe Shaibu baba aliyemleta mtoto wake kupata chanjo amewaomba wanaume wengine wajitokeze kwa majukumu hayo badala ya kuwaachia wanawake.

Related Posts