Geita. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita kimepata pigo baada ya diwani wake wa Kata ya Nyaruyeye Halmashauri ya Geita, Malimi Saguda kufariki dunia.
Malimi ameshika nafasi ya udiwani kwa vipindi viwili mfululizo na amefikwa na mauti akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Bugando kwa ugonjwa wa nimonia tangu Novemba 23, 2024.
Ni miezi minne imepita tangu diwani mwingine wa baraza hilo, Peter Kulwa aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari apoteze maisha.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashuri ya Geita, Charles Kazungu amesema kifo hicho kilitokea jana Desemba 5, 2024 wakati akipatiwa matibabu jijini Mwanza.
“Ameugua kuanzia Novemba 23, 2024 alilazwa Hospitali ya Waja baadaye alipewa rufaa akaenda Hospitali ya Kamanga ambao nao walimpa rufaa akaenda Bugando alikoendelea na matibabu hadi mauti yanakuta,” amesema.
“Alikuwa akisumbuliwa na Kisukari lakini kilichompeleka hospitali ni tatizo la mapafu, alikuwa na nimonia kali ambayo madaktari wamepambana kumuokoa lakini safari yake ikawa imefika mwisho, kutuachia pigo,” amesema Kazungu.
Kazungu amesema diwani huyo aliyehudumu kwenye nafasi hiyo kwa mihula miwili, alikuwa mwenyekiti wa kamati ya elimu, afya na maji na kwamba baraza limepoteza mtu muhimu aliyekuwa jasiri na mwenye kusimamia anachokiamini bila kuyumbishwa.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Geita, Gabriel Nyasilu ameiambia Mwananchi kuwa kifo hicho ni pigo kwa chama hicho.
Malima atazikwa nyumbani kwake Nyaruyeye Jumatatu ya Desemba 9, 2024.