Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi ameeleza changamoto tano walizoziona kwa upande wa sheria kwa kipindi cha miaka saba akiwa kwenye timu maalumu ya majadiliano ya Rais kwenye upande wa sheria na uandikaji wa mikataba ya kimataifa.
Profesa Kabudi ameeleza hayo leo Ijumaa, Desemba 6, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha Wanasheria wa Serikali kikao kilichoandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
Profesa Kabudi amesema yapo mambo mengi ambayo waliyabaini wakati wanafanya kazi kwenye timu hiyo likiwemo la baadhi ya watendaji wa taasisi za Serikali kutokuwa na uelewa wa namna ya utekelezaji wa baadhi ya masharti yaliyomo katika hati za makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali na wawekezaji kwa hivyo yalikuwa yanawatia hofu wawekezaji.
Amesema hiyo inatokea kwa sababu watendaji hao hawaelewi na wanapozungumza na wawekezaji badala ya kuwafafanulia waelewe, wajue sheria wao wanawaongezea hofu.
“Kumbe lilikuwa ni jambo la kufafanua, jambo la kueleza jambo la kuweka sawa, matokeo yake sasa tumeruhusu tafsiri nyingi za sheria zisizokuwa sahihi kuzagaa,” amesema Profesa Kabudi.
Amewataka wanasheria hao kama kuna jambo ambalo hawalielewi au kulifahamu vizuri hakuna sababu ya kuonyesha wanajua na badala yake wanatakiwa kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata ufafanuzi.
Kukabiliana na hilo, ameweka msisitizo kwa wanasheria hao kutotoa majibu ya haraka kama hawaelewi jambo badala yake wanatakiwa waombe wapewe muda wa kwenda kushauriana na wenzake na mwisho kabisa warudi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
“Sasa tumekuwa na tafsiri nyingi zisizokuwa sahihi za sheria zetu na tumejenga taswira ya kwamba sheria zetu zina upungufu mwingi ambao haupo, kwa sababu huo unaoonekana ni upungufu, ni upungufu wa sisi kuelewa lakini kutokukubali kwamba hatuelewi na kutokuelewa kwetu,” amesema Profesa Kabudi.
Amesema jambo jingine alilolibaini kwa kipindi hicho ni uchache wa wataalamu mahiri wa majadiliano na waliobobea katika maeneo mbalimbali.
Amesema hiyo inatokana na wanasheria wengi wamefundishwa kuwa kazi yao ni kushtaki na kusimamia kesi, lakini wanapotakiwa kwenye meza ya majadiliano wanapwaya kwa sababu hawana weledi kwenye upande huo wa majadiliano.
Pamoja na hayo Profesa Kabudi amesema kuna pengo kwenye kubaini ujanja, mbinu na hila za ukwepaji kodi, uhamishaji wa faida kwa kutumia mitandao ya makampuni yaliyoundwa katika maeneo, ambayo ni mahususi kwa ukwepaji wa kodi na uhamishaji wa faida.
Jambo jingine ni uvamizi wa maeneo ya leseni au maeneo ya ardhi na kuingia makubaliano na mwekezaji kwa lengo la kulipwa faida kwa mtindo wa tegesha kwa sababu baadhi ya mashauri mengi wanayoyapata hivi sasa yanayohusu ardhi ni watu wanajua eneo fulani yatapita maenedeleo fulani wanawahi halafu wanategesha.
Jambo jingine walilolibaini ni makampuni kusisitiza kuendelea kutumia mahakama za nje kwa masuala ya usuluhishi wa migogoro na sisi kutokuwapa maelezo ya mashauri ambayo yapo na yametatuliwa ndani ya nchi na bado wawekezaji wakashinda.
“Tulikuwa na shauri la barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo ambapo usuluhishi ulifanyika Tanzania na Mahakama Kuu ya Tanzania ilikubali ile tuzo sasa tukiwaeleza aina hiyo ya maeneo ambayo wamefanya mashauri yao hapa wakashinda na Serikali ikalipa fidia, kama ilivyo utaratibu tutajenga imani ya kuendelea kuimarisha mtindo wetu,” amesema Profesa Kabudi.
“Mengine tuliyoyaona ni kwamba yapo matatizo ndani ya watendaji wa Serikali ambao wanadhani mwanasheria anahitajika tu panapokuwepo mgogoro wa kisheria kwa hiyo wakati wa maandalizi ya majadiliano mwanasheria hatafutwi. Wakati wa majadiliano mwanasheria hatafutwi au hata akishirikishwa anashirikishwa juu juu, lakini inapotokea mgogoro sasa mwanasheria anaitwa afanye miujiza na asipofanya miujiza yeye ndiye aliharibu na yeye ndiye analaumiwa na kubeba mzigo.
Amesema moja ya njia za kuepuka migogoro ni Serikali kuwa makini kutekeleza makubaliano ya kimkataba baina ya Serikali na serikali za nchi nyingine au Serikali na kampuni za kimataifa hususani masharti ambayo yakivunjwa au kutozingatiwa ipo athari za kushtakiwa katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi.
Mikataba hiyo ni pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo mataifa ya kigeni yameingia na Serikali kwa lengo la kulinda mali na kuhifadhi maslahi ya wananchi wa mataifa yao.
“Wawekezaji hawaji hapa kama wahisani lakini pia nchi zetu hazipo hapa kuendelea kudhulumiwa, kwa hiyo ni lazima tuje na hilo kuhakikisha kuwa kila upande unanufaika,” amesema Profesa Kabudi.
Amesema taasisi za Serikali zinapaswa kutambua kwamba makubaliano yoyote baina ya Serikali na nchi nyingine na wawekezaji ni makubaliano ambayo yanaifunga nchi na Serikali yake kisheria na kwamba kila chombo au taasisi kwa kadri ya kuhusika kwake katika utekelezaji inapaswa kuzingatia makubaliano hayo.
Amesema kwa sasa wametoa angalizo kwamba umuhimu mkubwa uwekwe kwenye majadiliano kwa sababu kazi isipofanyika vizuri kwenye majadiliano watapata mikataba na makubaliano yanayowafunga kisheria ambayo hawataweza kukwepa
“Kwa hiyo umakini mkubwa uwe kwenye majadiliano kwa sababu tukiharibu kwenye majadiliano gharama yake tutailipa mbele ya safari.
“Ndiyo maana bado tutafikisha suala hilo la kuwa na chombo maalumu cha kusimamia mikataba ili mapema kabisa kubaini maeneo ya migogoro na kutafuta njia ya kuyamaliza mapema bila kulazimika kwenda mahakamani,”
Amesema kwa sasa dira na malengo la mijadala iwe ni kupata njia mbadala ya fidia kama vile kutoa njia nyingine badala ya wakati wote kwenda katika majadiliano hayo. Pia watumie njia za kidiplomasia za kutatua baadhi ya hii migogoro.
Amewataka wanasheria hao wa Serikali kutambua kuwa wanaitumikia Serikali na wananchi wake na Serikali ni moja tu hivyo hawana budi kushirikiana kwenye majukumu yao.
Mbali na hilo amewataka wanasheria hao kuheshimu maamuzi yanayotolewa na mahakama ili kujenga imani kwa wananchi badala ya kutotekeleza uamuzi unaotolewa na mahakama na kama kuna kutokuridhika na uamuazi huo wafuate taratibu za rufaa.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema katika kikao hicho wataangalia ni namna gani wataweza kufanya majadiliano, uandishi na usimamizi wa mikataba hasa ile ya kimataifa.
“Changamoto siwezi kusema ni kubwa kiasi hicho la msingi ni namna gani mnakumbushana jinsi ya kufanya usimamizi na majadiliano na namna ya kuandika mikataba hiyo hasa ile ya kimataifa ili kupunguza changamoto zote ambazo zinaweza kujitokeza, na siyo kwenye eneo hilo tu bali na maeneo mengine ambayo yanaweza kujitokeza kwenye eneo la sheria,” amesema Johari.
Amesema kwa sasa wanawekeza nguvu zaidi kwa wanasheria wa halmashauri kwa kuwa wao ndiyo wako karibu zaidi na wananchi.
Amesema kikao hicho kitawawezesha kuzungumza masuala mbalimbali yanayowahusu kwenye sekta ya sheria hasa ushirikiano baina yao.
Naye Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi amesema ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatoa mchango mkubwa kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria ambapo kwa sasa wanasimamia masuala yote ya mashauri ambayo Serikali imeshtaki au imeshtakiwa.