Kagoma aibuka, avunja ukimya ishu ya Simba

YUSUPH Kagoma ndilo jina linalotajwa sana kwenye mitandao ya kijamii hivi sasa na hii ni baada ya staa huyo wa Simba kufuta utambulisho wake na timu hiyo kwenye mtandao wake wa kijamii ‘Instagram’.

Sakata hilo limeenda sambamba na kuachwa Dar es Salaam wakati Simba ikiondoka nchini Jumatano alfajiri kwenda nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Costantine utakaopigwa Jumapili.

Baada ya sintofahamu hiyo Mwanaspoti imefanya mazungumzo na Kagoma jijini Dar es Salaam, akafafanua mambo kadhaa na sababu za kufanya hivyo huku akisisitiza baadhi ya mambo yanayosemwa mitandaoni kwa sasa sio ya kweli.

Ameweka wazi kwamba sababu kubwa ya kujiondoa kwenye mitandao hususan Instagram ni kutaka kutuliza akili wala hakuna kingine chochote na mechi ijayo ataonekana uwanjani.

“Hakuna ishu yoyote nimeamua kuacha kutumia Instagram kwa muda. Mimi bado ni mchezaji halali wa Simba kwa mujibu wa mkataba niliosaini mwanzoni mwa msimu huu,” anasema mchezaji huyo ambaye amekuwa muhimili muhimu wa Simba katika mechi za hivi karibuni.

“Kuhusiana na suala la kubaki Tanzania wakati timu ipo nchini Algeria mimi nilikuwa naumwa nimerudi kuanza mazoezi siku nne kabla ya timu kusafiri hivyo sipo fiti,” ameongeza Kagoma huku akikanusha baadhi ya maandiko yanayoenea kwenye mitandao yakimhusisha na kutaka kuondoka Simba.

Itakumbukwa kwamba kabla ya kujiunga na Simba mapema msimu huu, mchezaji huyo alikuwa akihusishwa na Yanga na ikaripotiwa kwamba viongozi hao wa Jangwani walishaweka dau mezani Simba wakacheza karata nzito.

Kagoma anasema ameachiwa programu maalum Dar es Salaam kwaajili ya kujiweka fiti na anaweza akawa sehemu ya mchezo unaofuata wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien Desemba 15 utakaopigwa Uwanja wa Mkapa.

Amewatakia kila la kheri timu yake kuelekea mchezo wa Jumapili huku akiweka wazi kuwa anaimani na kikosi kilichosafiri kwenda Algeria kinaweza kufanya vizuri na kuipa Simba matokeo mazuri kwa kuzingatia pia na walivyojipanga kambini.

Kagoma hajaonekana uwanjani tangu Oktoba 19, mwaka huu alipopata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam pia ameweka wazi kwamba hata akichezeshwa beki anakiwasha vizuri tu.

“Nimezoeleka na kufahamika kutokana na kutumika zaidi kucheza nafasi ya kiungo lakini mimi ni mchezaji ambaye nimepata nafasi ya kucheza nafasi tatu uwanjani na zote kwa ubora,” amusema na kuongeza:

“Naweza kucheza kwa ubora kabisa nafasi ya beki wa kati na beki namba mbili ni nafasi ambazo nimepata nafasi ya kucheza nikiwa kwenye kikosi ambacho kinashiriki Ligi Kuu Bara sio kwamba nimecheza nikiwa madaraja ya chini.”

Kagoma anasema hata sasa ikitokea kocha wake akampanga nafasi hizo anaweza kucheza kwa ufanisi kwasababu soka ni mchezo ambao anaupenda na hachezi kwasababu ya kufundishwa anakipaji.

“Tanzania imebarikiwa kuwa na vipaji vya wachezaji wengi hasa nafasi ya kiungo hata ukifuatilia Ligi Kuu Bara unaweza kukubaliana na mimi kwani wachezaji wengi wanaofanya vizuri ni nafasi ya kiungo,” amesema na kuongeza:

“Pamoja na timu kubwa za Simba na Yanga kuwa na wachezaji wa kigeni kwenye nafasi hizo bado wanawachanganya na wazawa ambao pia wameonyesha uwezo mkubwa na wa kuvutia huku wakitajwa zaidi midomoni mwa watu.”

Kagoma ameasema kuna wageni ni wazuri hata ukiwafuatilia unabaini kuwa kuna utofauti lakini hicho hakiondoi ukweli kwamba na wao ni bora na wamekuwa wakitoa changamoto kwa wageni huku akimtaja Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuwa pamoja na kupewa wachezaji wengi wa kigeni kwenye nafasi yake bado ameonyesha kuwa na uhitaji kikosini na kucheza akiwa Yanga na sasa Azam FC.

“Sio Fei Toto pekee pia ukiangalia kuna Jonas Mkude na Mzamiru Yassin ni viungo wazawa ambao wameonyesha changamoto kwa mastaa wa kigeni wamekuwa bora na wanapata nafasi ya kucheza hii ni ishara tosha kuwa wazawa pia ni bora utofauti ni uraia tu.”

“Nimeanza kucheza Singida United ikiwa daraja la kwanza na baadaye ikapanda nikacheza misimu miwili baada ya kushuka niliondoka na kujiunga ni timu nyingine laki ni moja ya timu ambayo nimecheza misimu mingi zaidi,” amesema na kuongeza:

“Baada ya kutoka Singida United nilijiunga na Gwambina ambayo niliitumikia kwa miaka miwili uwezo niliouonyesha nikiwa na timu hiyo ndio uliwavutia Geita Gold ambao walinichukua na kunisainisha mkataba wa miaka miwili lakini nimewatumikia mwaka mmoja na nusu na baada ya hapo ndipo nilipochukuliwa na Singida Big Stars.”

ATAJA SABABU WASHAMBULIAJI KUPOTEA

“Waafrika ni wepesi wa kuridhika hii ndio sababu kubwa ya washambuliaji wetu wengi kushindwa kuwa na muendelezo wa ubora lakini uwezo wanao lakini wakishafunga mabao yao kumi wanaona wameshamaliza,” amesema.

“Washambuliaji wengi wa kizawa wakipata mafanikio msimu mmoja msimu unaopfuata huo ni wakiendeleza kile walichokifanya msimu uliopita hii ni kwa sababu wanaridhika haraka na kujisahau.”

Kagoma anasema hawashangai ni kawaida ya watu wenye ngozi nyeusi tofauti na wachezaji wa mataifa mengine makubwa ambao wanaamini katika kuendeleza ubora wao.

KUMBE ILIKUWA AWE DAKTARI

Kagome amesema kama binadamu alikuwa na ndoto zake za kimaisha na hapa anautaja udaktari wa binadamu.

“Ndoto yangu ilikuwa ni kuwa daktari nakumbuka tangu naanza shule nikiulizwa unasoma ili uwe nani jibu lilikuwa ni kuwa Daktari ili niweze kuwatibu wagonjwa,” amesema.

“Lakini soka lilichukua nafasi kubwa zaidi ya masomo pamoja na kufanikiwa kumaliza kidato cha nne lakini sikuweza kutimiza ndoto yangu na kujikuta nawekeza nguvu saidi kwenye mpira ambao pia nilikuwa naupenda.”

Kagoma amesema hajaingia kwenye soka kwa kushawishiwa na mtu yeyote au kuvutiwa na mchezaji aliamua kuingia huko kutokana na mapenzi yake binafsi na mchezo huo.

“Ntakuwa  muongo nikisema nilivutiwa na mchezaji kwani nimeanza kucheza nikiwa na umri mdogo na kipindi hicho ata muda wa kuangalia mpira kw runinga ulikuwa hakuna kutokana kukosa muda kutokana na kuwa na mambo mawili kwa wakati mmoja kusoma na kucheza.”

KIKOSI CHAKE CHAMA, MAYELE NDANI

Kiungo huyo anataja kikosi chake bora ambacho amekiri kuwa kikitokea kikawa pamoja na kushiriki Ligi Kuu Bara hakuna timu inaweza kuwafunga akianza na kipa Khomen Abubakar, Shomari Kapombe, Shafiki Batambuz, Oscar Masai, Juma Nyosso, Yusuph Kagoma, Ayub Lyanga, Kenny Ally Mwambungu, Fiston Mayele, Clatous Chama na Pape Sakho.

“Kikosi hili ukifungwa chache tano mana kimekamilika kila idara ukuta wa chuma eneo la kiungo kuna watu ukiangalia mbele badi kuna Chama mtu wa maudhi kwenye chenga, kuna Mzee wa kutetema na Sakho mtu wa kukimbiza,” amesema na kuongeza:

“Ubora wa kikosi hiki kitaongezewa nguvu na kocha Hans Van Pluijm ambaye ni muumini wa kuchezea mpira hivyo nina imani kubwa kuwa kikiwa chini yake hakuna timu ya kutuzuia.”

“Nimepita chini ya makocha wengi lakini kocha Fredy Felix ‘Minziro’(sasa Pamba Jiji) ni kocha ambaye pamoja na ubora wake kwenye majukumu yake ni namna ambavyo anafurahia kazi ya vijana wake wawapo uwanjani,” amesema na kusisitiza:

“Nimekuwa nikimfuatilia kocha wangu hata nikiwa uwanjani ni mwalimu ambaye anakuwa na mikiki mikiki kama na yeye yupo uwanjani anacheza mshambuliaji akiwa kwenye harakati ya kutaka kufunga kwa mguu basi na yeye atafanya kama anapiga au ikitokea ni kichwa pia ataonyesha ishara ya kupiga kichwa.”

Amesema ni kocha ambaye amekuwa bora kwenye kazi yake ni rafiki wa wachezaji pale wanapofanya vizuri na ni mkali mchezaji akishindwa kufuata kile alikuwa anatarajia kukipna akikifanya.

Related Posts