Kongo yapambana na ugonjwa usiojulikana – DW – 06.12.2024

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, waziri wa afya wa Kongo Samuel Roger Kamba, amesema kuwa wako katika hali ya tahadhari na kwamba wanachukulia tukio hilo kama kiwango cha janga linalohitaji kufuatiliwa. Kamba amesema katika vituo vya afya, wamehesabu watu 27 waliofariki.

Pia amesema miongoni mwa vifo hivyo 27, watu 17 walikufa kutokana na matatizo ya kupumua, na kumi kwa ukosefu wa damu. Waziri huyo ameongeza kuwa vifo vingine 44 vimeripotiwa katika jamii lakini  sababu nyingine zinaweza kuchangia matukio hayo.

Ugonjwa usiojulikana nchini Kongo umesababisha vifo vya watu kadhaa.

Wakati wa mkutano kwa njia ya mtandao na kituo cha udhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika (CDC)  mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Umma Dieudonne Mwamba, alisema hawajui kama wanakabiliana na ugonjwa unaosababishwa na virusi ama bakteria. Mkuu wa shirika hilo la CDC barani Afrika, Jean Kaseya pia amesema hawatambui njia za maambukizi ya ugonjwa huo.

“Matumaini yetu, nasema matumaini yetu, kwanza tupate sampuli bora, pili sampuli zitakapofika, zitapelekwa kupimwa mkoani Kikwit, matokeo yataakisi ukweli wa mambo yanayoendelea katika eneo hili. Kwasasa hatuwezi kutoa maoni zaidi. Ikiwa tutatoa maoni zaidi juu ya hilo, itakuwa tu kueneza uvumi,” alisema Kaseya. 

Ugonjwa usiojulikana unasemekana kushika kasi katika eneo la Panzi

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Ugonjwa huo usiojulikana umekithiri katika eneo la Panzi, kilomita 700 kusini mashariki mwa mji mkuu wa Kongo, Kinshasa.Picha: GLODY MURHABAZI/AFP

Ugonjwa huo uliogunduliwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwezi Oktoba, sasa umekithiri katika eneo la Panzi, takriban kilomita 700 kusini mashariki mwa mji mkuu wa Kongo, Kinshasa. Ufikiaji wa eneo hilo kwa barabara ni wa kutatiza. Eneo hilo pia lina ukosefu wa miundo mbinu ya afya, na wakazi pia wanakabiliwa na uhaba wa maji ya kunywa na dawa.

Kamba amesema kuwa timu za wataalamu wa magonjwa zimetumwa Panzi kuchukuwa sampuli lakini wameondolea mbali hofu ya virusi vya corona na kuhitimisha kuwa ugonjwa huo unaathiri mfumo wa kupumua .

Ugonjwa usiofahamika wauwa watu 143 DRC

Kamba anasema zaidi ya asilimia 60 ya watu katika eneo hilo pia wanakabiliwa na utapiamlo, hasa watoto, na kufanya eneo hilo kuwa moja ya maeneo yenye viwango vya juu zaidi vya hali hiyo. Waziri huyo ameongeza kuwa miaka miwili iliyopita, eneo hilo tayari lilikuwa limekabiliwa na janga la homa ya matumbo.

Kulingana na takwimu za awali, ugonjwa huo ambao haujatambuliwa huathiri watoto wadogo, huku asilimia 40 ya maambukizi yakiwapata watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.

Chanzo: afp/ap
 

Related Posts