Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu anatajwa kuwania uenyekiti wa Taifa wa chama hicho, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani, Mwananchi imejulishwa.
Nafasi hiyo imeshikiliwa na Freeman Mbowe tangu mwaka 2004 akimrithi Bob Makani aliyeshika usukani kutoka kwa Edwin Mtei.
Mbowe sawa na Makani na Mtei, ni miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho mwaka 1992.
Taarifa kwamba Lissu anajitosa katika kinyang’anyiro hicho, imekuja kipindi ambacho amekuwa akitoa kauli tata kwa chama na hata viongozi wake.
Miongoni mwa kauli hizo ni za kukihusisha chama hicho na kashfa za rushwa.
Alianza kutoa madai hayo Mei 2, 2024 alipohutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, alikoeleza kuna fedha zimemwagwa zinazoweza kuharibu uchaguzi wa ndani wa Chadema.
Lissu pia amekuwa akikosoa hatua ya chama hicho kuingia maridhiano na CCM akidai kilidanganywa.
“Tumedanganywa tukadanganyika, tumeletewa lugha laini ya uongo ya maridhiano. Tukaingiziwa vijineno vinavyosema hivi, msiwe wakali sana mtapewa Serikali ya nusu mkate,” alisema Lissu Novemba 12, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari mjini Singida.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alikanusha madai hayo, akisema Chadema haijawahi kuletewa hoja ya kugawana madaraka kutoka chama chochote. Pia alikana madai ya rushwa akieleza hakuna ushahidi uliotolewa.
Kukiwa na taarifa kutoka kwa watu wake wa karibu kwamba Lissu ana mpango wa kuwania uenyekiti wa Chadema, mwenyewe alipotafutwa na Mwananchi leo Desemba 6, 2024 amesema: “No comment ( sina la kusema).Ninachotaka kukwambia ni kwamba, wakati utakapofika nitakujulisha au utajulishwa,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi Mei 5, 2024 kuhusu madai ya kuwepo kwa mvutano kati yake na Mbowe, Lissu alipinga kuwa na mpango wa kugombea uenyekiti.
“Mimi sina mpango wa kugombea uenyekiti wa Chadema. Kwa miaka minane nimekuwa nikisema hivyo, mnataka niseme mara ngapi? Watu wanaosema hayo ni wajinga,” alisema.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa vyanzo vya uhakika zinasema mpango wa Lissu kugombea uenyekiti umeiva. Inaelezwa ilikuwa atangaze nia Desemba 7, lakini imeahirishwa hadi itakapotangazwa tena.
“Ilikuwa iwe hivyo, lakini tumeahirisha kwa sababu kuna vikao vinaendelea, tutawajulisha tarehe ya tukio,” amesema mmoja wa watu wa karibu na Lissu.
Mmoja wa viongozi wa Chadema wa kanda mojawapo, amelieleza Mwananchi kuwa alialikwa kwenye mkutano wa Lissu kutangaza nia.
“Nimepigiwa simu kualikwa kwenye kikao cha kutangaza nia ya uenyekiti,” amesema aliyeomba kutotajwa jina.
Tangu uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024 ambao ulilalamikiwa na Chadema kutokana na wagombea wake kuenguliwa pamoja na dosari nyingine, chama hicho hakijatoka hadharani kutoa tamko.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema Novemba 28, ilisema Kamati Kuu ya chama hicho ingeketi Novemba 29 chini ya uongozi wa Mbowe na baada ya kikao hicho tamko lingetolewa.
Novemba 30, 2024 kwa mujibu wa taarifa ilizozipata Mwananchi zilisema kikao kilifanyika awali kwa njia ya mtandao wa Zoom, lakini iliafikiwa kutokana na uzito wa suala la uchaguzi wajumbe wakutane ana kwa ana jijini Dar es Salaam.
Hivyo kikao hicho kiliahirishwa hadi Desemba 2, 2024. Taarifa zinasema katika kikao hicho kuliibuka mvutano miongoni mwa wajumbe kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama hicho, huku suala la uchaguzi wa serikali za mitaa likiwekwa kiporo na jukumu hilo kuachwa kwa viongozi wakuu kulijadili na kisha taarifa itolewe kwa umma.
Kutokana na yanayoendelea ndani ya chama hicho, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus anaeleza ni dalili ya mpasuko.
“Ikumbukwe kuwa Lissu anaungwa mkono na vijana zaidi na Mbowe anaungwa mkono zaidi na Bawacha (Baraza la Wanawake la Chadema) na Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha) pamoja baadhi ya wajumbe wa kamati kuu.
“Nadhani waruhusu demokrasia ichukue mkondo wake ndani ya chama. Mchakato mzima wa uchaguzi usiwagawe viongozi wa ngazi ya juu na wanachama wao,” amesema.
“Pia wanachama waachwe huru kuchagua viongozi wao na kusiwepo na hujuma, mwenyekiti aliyepo madarakani (Mbowe) akubali kuruhusu wanachama wengine washindane naye kwa uhuru kwa masilahi mapana ya chama chake,” amesema.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa UDSM, Dk Richard Mbunda amesema huenda uamuzi wa Lissu usipokewe vizuri na hivyo kuleta mtikisiko.
“Likitokea hili tunaweza kushuhudia Lissu akiondoka Chadema na hizi fununu zimekuwepo kwa muda sasa.Kama wakiridhia kwenda kwenya uchaguzi, basi wanachama watawekwa njia panda au kuendelea na Mbowe au kwenda na Lissu,” amesema.
Dk Mbunda amesema Chadema kinapaswa kuliishi jina lake kama chama cha demokrasia na kuruhusu demokrasia ya ndani itawale, akisema mchakato huo utawapa uhalali wa hali ya juu.
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (alizaliwa Januari 20 1968 katika Wilaya ya Ikungi, Singida. Ni mwanasheria na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) tangu mwaka 2019.Pia, ni Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Tundu Lissu alizaliwa katika kijiji cha Mahambe, wilaya ya Ikungi, Tanzania. Alisoma Shule ya Sekondari ya Ilboru jijini Arusha na kuhitimu mwaka 1983 na baadaye Galanos mkoani Tanga.
Alipata shahada ya kwanza ya sheria (LLB) kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam na baadaye shahada ya uzamili katika sheria (LLM) katika Chuo Kikuu cha Warwick nchini Uingereza kati ya 1995 -1996.
Alifanya kazi na Lawyers Environmental Action Team (LEAT) na pia World Resources Institute kama mwanasheria. Alijihusisha na masuala mbalimbali ya haki za ardhi, hasa katika maeneo yaliyohifadhiwa na sekta ya madini.
Aliwahi kugombea ubunge katika jimbo la Singida Mashariki kupitia NCCR Mageuzi mwaka 1995 lakini hakufanikiwa.
Mwaka 2009 alijiunga na Chadema na mwaka 2010 aligombea tena ubunge katika jimbo hilo na kushindwa.
Kwa miaka mingi, Lissu amejijengea sifa kama mwanasheria mashuhuri, kiongozi wa upinzani mwenye ushawishi mkubwa na mkosoaji wa Serikali.
Alijipambanua zaidi kwa kukabiliana mara kwa mara na Serikali wakati wa utawala wa Rais John Magufuli.
Kutokana na kauli zake na upinzani wake, amejikuta kwenye mikasa mingi.
Septemba 7, 2017, Lissu alivamiwa na watu wasiojulikana na kupigwa risasi 16 baada ya kutoka bungeni akielekea nyumbani kwake Area D, Dodoma.
Baada ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali rufaa ya Dodoma kabla ya kusafirishwa kwa ndege hadi hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Alilazwa huko kwa miezi minne kabla ya kuhamishiwa Ubelgiji kwa ajili ya matibabu zaidi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven huko Gasthuisberg.
Mwaka 2020 alirejea nchini na kugombea urais kupitia Chadema katika uchaguzi ambao chama hicho ulilalamika kutokuwa wa haki.
Freeman Aikaeli Mbowe aliyezaliwa Septemba 14, 1961 ni mfanyabiashara na mwanasiasa, akishika nafasi ya uenyekiti wa Chadema Taifa tangu mwaka 2004.
Ni mmoja wa waanzilishi wa Chadema mwaka 1992. Uwezo wake wa kuwa na mkakati mzuri wa kisiasa umemfanya kuwa mmoja wa wanasiasa muhimu ndani ya chma hicho, akikikuza kutoka chama kidogo hadi chama chama kikuu cha upinzani, kikikusanya idadi kubwa ya wanachama na kupata wabunge, madiwani na viongozi wa serikali za mitaa.
Aliwahi kuwa mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro mwaka 2000 hadi 2005 na pia alishika nafasi hiyo kuanzia mwaka 2010 hadi 2020.
Mwaka 2005, Mbowe aliteuliwa kuwa mgombea urais wa Chadema. Katika uchaguzi huo Mbowe alishika nafasi ya tatu nyuma ya Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, huku Jakaya Kikwete wa CCM akishinda na kuwa rais wa awamu ya tatu.
Julai 2021, Mbowe alikamatwa pamoja na wanachama wengine kumi wa Chadema wakiwa jijini Mwanza kwa ajili ya maandamano.
Serikali ilimshtaki ikimtuhumu kwa ugaidi, na alikaa gerezani kwa karibu mwaka mzima kutokana na mashtaka hayo ambayo hayaruhusu dhamana nchini Tanzania.
Machi 2022, mashtaka ya ugaidi dhidi yake yalifutwa na waendesha mashtaka wa Serikali na baada ya kuchiliwa kutoka gerezani, siku hiyo hiyo alikutana na Rais Samia Suluhu Ikulu ya Dar es Salaam.
Baada ya kikao chao walianzisha mazungumzo ya maridhiano kati ya CCM na Chadema, ambayo hata hivyo baada ya vikao kdhaa yalivunjika.