Arusha. Katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, Hospitali ya Rufaa Mount Meru imeitisha kambi ya madaktari bingwa kwa ajili ya kuwapa fursa wananchi wa mkoa wa Arusha wenye changamoto za kiafya kupata huduma za kitabibu bure.
Kambi hiyo yenye kaulimbiu ‘miaka 63 ya Uhuru, imarisha Afya kwa kunufaika na mapinduzi makubwa ya uboreshaji wa huduma za Afya’ inafanyika kwa siku nne ndani ya Hospitali ya Mount meru kuanzia leo Desemba 6 hadi Desemba 9, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 6, 2024, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Mount Meru, Dk Alex Ernest amesema kambi ina madaktari zaidi ya 30 wanaotarajiwa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 4,000 wenye changamoto mbalimbali za kiafya.
Amesema kambi hiyo itatoa huduma bure kwa wagonjwa wote kuanzia kumuona daktari, vipimo vya maabara, vipimo vya jiolojia (X-Ray), na vipimo vya kumulika (Ultra sound).
“Katika kambi hii iliyoanza leo kuna madaktari bingwa na wabobezi wa mkoa mzima wa magonjwa yote ya watoto na wanawake pia matatizo ya uzazi, njia ya mkojo, saratani, pua, koo, macho na sikio” amesema Dk Alex.
Amesema huduma hizo zote zitaenda sambamba na kupewa dawa na miwani kadri itakavyohitajika lakini zaidi watafanya huduma ya upasuaji kwa majeraha ya ajali na mifupa.
“Pia kuna kitengo maalumu cha kusaidia watu kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na watakaokutwa na magonjwa hayo watatibiwa na watapewa elimu ya kubadilisha mtindo wa maisha ili kujikinga,” amesema.
Lengo la kambi hiyo, Dk Alex amesema ni kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania ambayo wanataka kuwaonesha wananchi jinsi Serikali ilivyowekeza katika miundombinu ya kuboresha huduma za afya nchini na uwezo wa wataalamu wa ndani, hivyo hawahitaji tena kuingia gharama za kwenda nje kutibiwa.
“Lakini pia tunalenga kuwafikia wananchi wasio na uwezo wa kifedha wa kupata huduma za kibingwa ambao wamekuwa wanapoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama,” amesema na kuongeza.
“Pia kusogeza hospitali karibu na wananchi wajue huduma tunazotoa kwa haraka na ukaribu, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha umuhimu wa afya bora katika miaka 63 ya Uhuru kwa kupima afya mara kwa mara” amesema.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kuhakikisha wanatumia fursa ya kambi hiyo kupata huduma za afya na kupima afya zao kwa uhakika zaidi wa maendeleo ya afya zao.
Saidi Bakari, mkazi wa Sanawari aliyehudhuria kambi hiyo amesema mpango huo ni mzuri na umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani ambao wamekuwa wakitumia fursa.
“Shida sio kupima mara kwa mara, tatizo ni gharama na uchumi ni mgumu mfukoni, hivyo tunaomba Serikali kuweka mpango wa huduma hizi mara kwa mara ili kusaidia wananchi wasio na kipato kikubwa kupata uhakika wa afya zao,” amesema.
Salma Mongy mkazi wa Sinoni aliyetibiwa macho na kupewa miwani amesema alishawahi kuandikiwa miwani hiyo ya Sh150,000 lakini kutokana na uwezo mdogo wa kifedha alikosa na kuendelea kuugulia maumivu kabla ya leo kupewa miwani hiyo bure.
“Macho huwa yananisumbua hasa kipindi cha vumbi, mwanga mkali hasa jua na katika kuja kupima nikaandikiwa miwani ya Sh150, 000 mwezi Septemba, lakini sikuweza kununua kutokana na kipato changu, nashukuru leo nimepata” amesema.