Arusha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewaonya wajumbe wa tume ya wataalamu ya uchunguzi wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne Kariakoo jijini Dar es Salaam, kutokulindana na kuwaficha wahusika wa uzembe uliosababisha ajali hiyo.
Aidha amesema ripoti ya tume hiyo haitasaidia eneo la Kariakoo peke yake bali itatumika kote nchini kusimamia ujenzi uwe bora na salama.
Akizungumza jijini Arusha, leo Ijumaa Desemba 6, 2024, katika Kongamano la kimataifa la Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Majaliwa amesema hawatarajii mtu yoyote kulindwa na tume hiyo, badala yake wanatarajia kupata ukweli wa kilichotokea.
Amesema wako baadhi ya wahandisi ambao wanaichafua taaluma hiyo kwa kufanya matendo ambayo ni kinyume na maadili ikiwemo rushwa, ubadhirifu na ukosefu wa weledi na kuwa hiyo si kwamba inachafua taaluma hiyo pekee bali inaharibu taswira ya nchi.
“Nichukue mfano wa jengo lililoporomoka la Kariakoo, ingawa bado hatujapata matokeo, ila kwa harakaharaka unaona kuna tatizo la mwendelezo wa ujenzi na pale Jiji kuna wahandisi, mtu anapochokonoa chini ya ardhi kwenye jengo ambalo halikujengwa kwa mpango ya kuchokonoa kujenga hiyo basement,” amesema.
“Tutapata matokeo na bahati nzuri tumewapa nafasi nyie kuunda tume hiyo, tunatarajia hamtamlinda mtu pamoja na kwamba wote wale ni wanataaluma yenu, mtakuwa wakweli kueleza nini kimetokea na mtamtaja kila aliyehusika katika kuruhusu hali ile kutokea,” amesema.
“Sisi tunaamini wahandisi ni watu waaminifu lakini taaluma yenu ni taaluma ambayo ina heshima duniani siyo Tanzania tu, na tume ikishakuja na matokeo na kueleza tatizo liko wapi, mapendekezo ya tume hayatasaidia Kariakoo tu, yatakwenda mpaka mikoani kusimamia ujenzi bora,” ameongeza.
Waziri Mkuu amewataka wahandisi hao wanapoona kuna maeneo yanahitaji mabadiliko ya sheria au kanuni yanayowafanya washindwe kutekeleza majukumu yao, wasiache kusema na Serikali itafanyia kazi mapendekezo hayo na kuweka mkazo wa kuimarisha taaluma hiyo.
Akizungumzia hilo, Mjumbe wa Bodi ya Usajili Wahandisi (ERB), Ngwisa Mpembe, amesema ajali ya Kariakoo inawakumbusha, kwa namna yenye maumivu, umuhimu wa kuwa na wahandisi na wataalamu wa ujenzi wenye sifa na kuhakikisha watu wasio na sifa za uhandisi hawafanyi shughuli za kihandisi kama ujenzi.
Kuhusu ajali za barabarani, Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akielekeza Jeshi la Polisi kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha usalama barabarani unapewa kipaumbele na mamlaka nyingine.
Amesema kuna baadhi ya halmashauri vizuizi walivyoweka barabarani kwa ajili ya kukusanya mapato vinasababisha ajali na kuathiri watumiaji wengine wa barabara.
“Eneo hili haliwagusi sana, ila linakwaza vipimo vyenu, nyie mnajenga barabara sijui mita saba sijui tisa, halafu anakuja mkurugenzi wa halmashauri anaweka kizuizi zinazozuia barabara halafu anaacha sehemu ndogo ya kupita, polisi mnaona kizuizi badala ya kutumia barabara yote anawaachia nusu.
“Anayemuhitaji ni dereva wa lori aliyebeba mahindi kutoka kwenye halmashauri yake, hivyo kwa nini asiache barabara wazi akawa anasubiri lori unalipungia mkono unalisimamisha unakagua linapita, barabara ibaki, itumike inavyopaswa,” amesema
Ili kudhibiti ajali za barabarani amewataka wataalamu wa miundombinu kutoa mapendekezo ya kitaalamu kuhusu matumizi sahihi ya barabara ili kuhakikisha usalama wa wananchi unakuwa kipaumbele.
“Tumekuwa mashuhuda wa athari mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani matumizi ya barabara zetu tulizojenga na maeneo mengine yenye kazi za kiuhandisi yameleta madhara makubwa,”
“Mfano huko barabarani tunaona ajali nyingi sana hivi tumeshajifunza kwa nini eneo hili kila siku litokee ajali, kwa nini barabara toka Dar es Salaam kwenda Morogoro kunakuwa na ajali nyingi za barabarani?” amehoji.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema wanaendelea kushirikiana kuhakikisha wakandarasi pamoja na wahandisi kwa kadiri inavyowezekana.