NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI NA UKANDA WA SADC KUENDELEZA TEKNOLOJIA YA MATUMIZI BORA YA NISHATI

Na Seif Mangwangi, Arusha

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki na za ukanda wa SADC zimekubaliana kuendeleza teknolojia ya matumizi bora ya Nishati ili kukuza uchumi wa wananchi wao pamoja na kutunza mazingira yanayoendelea kuharibiwa kwa kasi.

Hayo ni miongoni mwa maazimio yaliyokubaliwa katika mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati uliohusisha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliomalizika leo jijini Arusha.

Mkutano huo uliokuwa ukifanyika jijini Arusha kuanzia Desemba 4 hadi Desemba 5 ,2024 umefungwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo ambaye ameeleza kuwa umehusisha Watunga Sera, Sheria, Viongozi, Wataalam na Wabobezi katika masuala ya Nishati kwa lengo moja la kuwa na matumizi sahihi ya Nishati.

Dkt. Jafo amesema lengo la nchi hizo ni kuendelea kukuza uchumi, viwanda vifanye kazi na biashara zifanyike kwa ufanisi lakini hilo litawezekana ikiwa kuna nishati ya kutosha ambayo uwepo wake unategemea usahihi katika matumizi yake.

Ameeleza kuwa, Tanzania inatilia mkazo suala la matumizi bora ya nishati ambapo kwa sasa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaandaa viwango fanisi vya vifaa vya nishati vinavyozalishwa au kuingizwa nchi vitakavyowezesha nchi kutumia umeme kwa ufanisi.

Amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya Nishati na kusema uwekezaji huo una maana kubwa katika kuendeleza viwanda na biashara.

Pia ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kuratibu Mkutano huo wa Siku mbili kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati imejipanga kutekeleza Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati uliozinduliwa tarehe 4 Desemba 2024 kwa kuhakikisha Mkakati huo unatekelezwa kwa kuwekewa bajeti ili nchi iweze kuwa na ufanisi katika vifaa vya nishati.

Amesema kupitia mkutano wa REEC 2024 maazimio mbalimbali yamefikiwa ikiwemo kufanya tafiti za pamoja ili kuboresha matumizi bora ya nishati na kuihusisha kikamilifu Sekta Binafsi.

kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso ameipongeza Serikali kwa kuendesha na kusimamia vizuri mkutano wa REEC 2024 ulioleta mafanikio makubwa ikiwemo mafunzo na kubadilishana uzoefu ili kuwa na ufanisi kwenye matumizi ya nishati.

 

Related Posts