NENDENI MKALETE MAPINDUZI KWA KUSHUGHULIKIA MREJESHO KATIKA OFISI ZA UMMA-BI. LEILA MAVIKA

Na.Lusungu Helela- Dodoma

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI, Bi. Leila Mavika amewataka Waratibu wa Kushughulikia Mrejesho wakayatumie mafunzo waliyoyapata kuleta mapinduzi katika Madawati au Ofisi za Mrejesho zilizopo katika Taasisi zao ili kufanikisha ushughulikiaji mrejesho kwa ufanisi na kwa wakati katika Ofisi za Umma kwa vile wameaminiwa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi.

Amewataka wakawe waaminifu na wenye haiba inayokubalika na Wateja wa ndani na nje ya Taasisi ili kuwafanya Wateja wao kuwa huru kufikisha malalamiko yao bila ya kuwa na wasiwasi wa aina yeyote.

Bi.Mavika ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo maalum yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu kwa Waratibu wa Kushughulikia Mrejesho kuhusu uendeshaji wa mfumo wa e-Mrejesho katika Ofisi za Umma.

Bi.Mavika mewataka Waratibu hao kutoa fursa sawa kwa wananchi wote kwa kutumia mfumo wa e-Mrejesho ili kuwawezesha wateja kutuma malalamiko, pongezi pamoja na maulizo kwa Serikali mahali popote na wakati wowote.

Aidha, Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu,UTUMISHI, Bi.Mavika amewaonya Waratibu hao kuacha tabia ya kushughulikia mrejesho wa wananchi mara tu wanaposikia kuna ukaguzi maalum kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

” Nendeni mkawe kioo fanyeni kazi muda wote, hatutegemei kuona mnashughulikia mrejesho kutoka wananchi mara tu mnaposikia kuna ukaguzi maalum” amesisitiza Bi.Mavika.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Janeth Mishinga ameeleza kuwa licha ya Waratibu hao kupewa mafunzo hayo ya kushughulikia mrejesho kwa wananchi kwa wakati pia wamepewa mafunzo ya mbalimbali ya kuwafanya kuwa Watumishi wa mfano katika jamii
Naye Mwenyekiti wa Waratibu wa kushughulikia Mrejesho, Denis Gondwe akizungumza kwa niaba ya Waratibu hao amesema mafunzo hayo yamekuwa ni muhimu sana kwao ikizingatiwa kuwa shabaha ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kutoa huduma bora kwa wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Related Posts