MOHAMED Abdallah ‘Baresi’ wa Mashujaa ndiye kocha peee aliyesalia kwenye timu moja kwa muda mrefu katika vikosi vya sasa vya klabu za Ligi Kuu Bara, akidumu kwa zaidi ya siku 514 ikiwa ni sawa na miezi 16, tangu alipojiunga na timu hiyo msimu uliopita wa 2023/24.
Katika mazingira ya soka la kisasa, mabadiliko ya makocha ni jambo la kawaida, Bares amekuwa ni kielelezo cha uvumilivu na ushirikiano mzuri na uongozi wa timu.
Wakati msimu huu wa 2024/25 ulipoanza, walibaki makocha watano tu ambao waliendelea kuwa sehemu ya vikosi vyao.
Makocha hao ni Youssouph Dabo wa Azam FC, Miguel Gamondi wa Yanga, Abdulhamid Moallin wa KMC na David Ouma wa Coastal Union na Baresi. Kwa upande mwingine, yalishuhudiwa mabadiliko 18 ya makocha kipindi cha msimu uliopita, jambo ambalo linathibitisha ugumu wa kazi hii ya ukocha na mabadiliko ya mara kwa mara yanayoshuhudiwa katika ligi.
Msimu uliopita, Singida Fountain Gate (kwa sasa ikijulikana kama Fountain Gate) ndiyo iliongoza kwa kutimua makocha na ilianza na Mholanzi, Hans van Pluijim, aliyeongoza timu hiyo kwa muda mfupi na aliyechukua nafasi yake ni Mjerumani, Ernst Middendorp, aliyeendelea kwa kipindi kifupi tu, akachukua nafasi Mbrazil Ricardo Heron Ferreira, naye pia aliondolewa muda mfupi. Baada ya hapo, Msauzi, Thabo Senong alichukua usukani.
Lakini hata yeye (Senong) alikosa mafanikio na kuondolewa kabla ya Jamhuri Kihwelo alikabidhiwa timu, lakini hata yeye alishindwa kuleta mabadiliko na alitimuliwa. Mwishowe, nafasi ya kocha ilichukuliwa na Ngawina Ngawina.
Msimu huu wa 2024/25, kuna mabadiliko ya makocha tena (11) wakati ligi ikiwa raundi ya 13, lakini hali ni tofauti kwa upande wa Mohamed Abdallah ‘Bares’.
Akizungumza kuhusu changamoto na mafanikio aliyonayo, Bares alieleza: “Kazi yetu ya ukocha ni ngumu sana. Binafsi, nashukuru kwa imani ambayo viongozi wa Mashujaa wamekuwa nayo juu yangu, tumekuwa tukifanya kazi kwa kushirikiana kuhakikisha timu inafanya vizuri.”
Kwa sasa, Mashujaa ipo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 17, ambapo wanashika nafasi ya nyuma kwa pointi nne tu dhidi ya Tabora United, ambayo inashika nafasi ya tano.