Nyota wa zamani wa Spurs,  West Ham kusaka vipaji Bongo

MSHAMBULIAJI na nyota wa zamani wa klabu za West Ham United na Tottenham za England, Frédéric Kanouté anatazamiwa kuja nchini ili kusaidia kutafuta vipaji kupitia mashindano ya soka kwa Vijana Afrika Mashariki ambayo itafanyika jijini Arusha.

Kanoute aliyewahi pia kutamba na Sevilla ya Hispania, Lyon ya Ufaransa na timu ya taifa ya Mali, akishinda tuzo za Mwanasoka Bora wa Afrika 2007 akiwaka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza aliyezaliwa nje ya bara la Afrika kushinda tuzo hiyo ataongoza jopo la kusaka vuipaji katioka michuano hiyo ya vijana.

Ujio wake katika mashindano hayo yanayojulikana kama Chipkizi Cup ambayo yanafanyika kwa mwaka wa 15 sasa, ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kutoa nyota wengi akiwemo beki wa Goztepe ya Uturuki na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Novatus Dismas unalenga katika kusajili wachezaji Chipukizi wenye vipaji.

Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Desemba 9 hadi 15 mwaka huu kwa kushirikisha zaidi ya timu 320 kutoka nchi za Afrika Mashariki na nyingine kutoka nje ambapo kwa mara ya kwanza timu za soka za Kafue Celtic inayoshiriki Ligi Kuu Zambia na Plateau United inayoshiriki Ligi Kuu Nigeria zitashiriki.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Future Stars Academy (FSA), Alfred Itaeli wanaoandaa  mashindano hayo ameithibitishia Mwanaspoti kuwa, Kanouté atakuwa ni miongoni mwa mawakala ambao watakuja kuangalia vipaji vya Soka na michezo mingine ambapo atawasili hapa nchini Disemba 11 mwaka huu.

Amesema ujio wake ni fursa kwa Soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kwani wachezaji ambao atawachagua watapata nafasi ya kutimiza ndoto za kucheza Soka la kulipwa barani Ulaya ambapo pia kwa miaka ya baadae watakuja kuwa matunda mazuri kwa timu zao za taifa.

“Kwetu ni furaha kuona tunazidi kuwa daraja kwa vijana kutimiza malengo na ndoto zao kikubwa tu wachezaji wote ambao watashiriki mashindano haya wapambane ili kupata nafasi ya kuchaguliwa,” amesema Itaeli.

Jumla ya wachezaji 4800 wa timu za vijana kuanzia umri wa chini ya miaka 9-20 kwa upande wa Wavulana na Wasichana watashiriki katika michuano hiyo ambayo itafanyika katika viwanja vya UWC, Agha Khan, St Constantine, TGT na Braeburn, huku ikishirikisha michezo ya Soka,Kuogela na Mpira wa Kikapu lengo kubwa ya michuano ikiwa ni kuibua na kukuza vipaji pamoja na kutangaza Utalii wa Tanzania kupitia michezo.

Related Posts