ROSTAM AZIZ: TUNALO JUKUMU LA KUWASAIDIA WATANZANIA KUJUA KUFANYA BIASHARA

Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, ametoa wito wa kuanzishwa kwa semina mikoani kwa ajili ya kuwaelimisha wafanyabiashara wadogo namna ya kufanya biashara kwa mafanikio, kupata mikopo, na kupanua shughuli zao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kikao cha “Roundtable” cha wafanyabiashara na wawekezaji wa Kitanzania, Rostam alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya uzoefu wa kibiashara kwa wafanyabiashara wadogo. 

Alieleza kuwa hakuna tofauti kubwa kati ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo, akibainisha kuwa yeye mwenyewe alikulia katika mazingira ya kawaida wilayani Nzega, mkoani Tabora, na alianza kuvaa viatu akiwa na umri wa miaka tisa.

“Nimetoka shule ya kijijini. Kama mimi nimeweza, Watanzania wengi wanaweza. Inatakiwa tuwasaidie, maana huwezi kuachia Serikali peke yake. Serikali inatunga sera nzuri, lakini nasi tunapaswa kushiriki kuwaongoza Watanzania wenzetu kufanikisha biashara zao,” alisema.

Aidha, Rostam alihimiza wafanyabiashara wakubwa kuwashirikisha wenzao wa Kitanzania katika fursa mbalimbali za kibiashara na kuhakikisha kuwa wanapata mafunzo ya kujiepusha na kufilisika.

Kauli ya Rostam imeibua mjadala wa umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali katika kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kukuza uchumi wa nchi.

Related Posts