Mwanza. Zaidi ya watoto wachanga 1,452 walifariki dunia mwaka 2023 mkoani Mwanza huku sababu ya kukosa hewa na maambukizi, zikitajwa kuchangia vifo hivyo.
Akizungumza Novemba 5, 2024 wakati wa uzinduzi wa programu ya utoaji huduma za afya kwa watoto wachanga (NEST360) katika halmashauri tano za Mkoa wa Mwanza, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk Silas Wambura amesema watoto hao walifia tumboni na wengine kufariki muda mchache baada ya kuzaliwa.
“Na sababu kubwa zinazochangia watoto hawa kufariki ni kukosa hewa, maambukizi na wakati mwingine wajawazito wanakuja wamechelewa kwenye vituo wakati wa kujifungua na wakati mwingine wanakuja vituo vya afya wakiwa wametumia dawa za kienyeji kuongeza uchungu,” amesema Dk Marwa.
Ameongeza kuwa wajawazito hao wanatumia dawa za kienyeji ili kuharakisha uchungu, hivyo dawa hizo zinawaathiri watoto wakiwa tumboni na wengine kufariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.
“Na wakati mwingine hizo dawa zinasababisha kizazi kuchanika na kuhatarisha uhai wa mtoto kabla hajazaliwa, wakati mwingine ni maambukizi kwa sababu wanapotumia hizo dawa wengine wanaziweka ukeni, zile dawa zinaleta maambukizi yanayoweza kuwapata watoto wanapozaliwa na kufariki muda mfupi baada ya kuzaliwa,” ameeleza Dk Marwa.
Dk Marwa amewataka wajawazito kuwahi vituo vya afya wanapohisi dalili za uchungu kwa kuwa kuchelewa kwao husababisha wakati mwingine mtoto kumeza maji ya tumboni na kukisababishia kichanga kupata shida ya upumuaji.
“Mtoto asipopata huduma ya haraka anaweza kufariki kwa sababu mfumo wake wa kupumua una changamoto, kwa hiyo mpango huu utasaidia kuondokana na vifo hivi kwa sababu kwanza utawajengea uwezo watumishi wetu, pili utatusaidia kununua vifaa na vifaa tiba ambavyo kwa maeneo mengine bado ni changamoto,” amesema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkazi wa NEST360 nchini, Dk Mariam Johari zaidi ya asilimia 80 ya watoto huzaliwa hospitalini, lakini bado watoto milioni 2.3 hufariki kila mwaka duniani.
“Asilimia 80 ya vifo hivi vinaweza kuzuilika. Tanzania imechukua hatua kubwa ya kupunguza vifo vya watoto wachanga ambavyo kwa mwaka 2004/5 vilikuwa vifo 32 kwa kila vizazi hai 1,000 na kupungua hadi vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2002. Ili kufikia lengo la Maendeleo Endelevu la kuwa na vifo vya watoto wachanga visivyopungua 12 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030, Tanzania inapaswa kuimarisha juhudi zake,” amesema Dk Mariam.
Amesema awamu ya kwanza mpango huo ulitekelezwa mkoani Dar es Salaam, Mbeya na Kilimanjaro ambapo vitengo vya huduma za watoto wachanga vilipanuliwa, kutoa vifaa muhimu vya huduma, pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya, awamu ya pili Zanzibar na Mwanza zikiongezwa.
“Katika awamu ya Pili nchini Tanzania, NEST360 imewekeza dola milioni 7.1 kusaidia juhudi za Serikali za kupunguza vifo vya watoto wachanga. Ufadhili huu utazinufaisha moja kwa moja hospitali 28. Hospitali 25 kati ya hizo ni katika mikoa minne ya Tanzania Bara na hospitali tatu Zanzibar,” amesema Dk Johari.
Amesema mpango huo unahusisha ukarabati miundombinu, ununuzi na utoaji wa vifaatiba, kujenga uwezo kwa madaktari na wahandisi wa vifaatiba ili kutoa huduma bora.
Akizindua mpango huo wa miaka minne kuanzia 2024 hadi 2028 katika Halmashauri za Buchosa, Sengerema, Misungwi, Nyamagana na Ilemala, Kaimu Katibu Tawala mkoani Mwanza, Chagu Nghoma amewataka wataalamu wa afya kutumia utaalamu wao ipasavyo kudhibiti vifo vya watoto wachanga.