Na Oscar Assenga,TANGA
Utafiti wa mafuta uliofanywa katika Bonde la Eyasi-Wembere, lililopo katika Bonde la Ufa la Afrika Mashariki umeelezwa kuwa utachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa taifa kwa kuongeza pato la taifa na kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka nje.
Hayo yalisemwa leo na Meneja wa Mradi wa Utafiti wa Mafuta katika Bonde la Eyasi-Wembere, Sindi Maduhu wakati wa mkutano wa wanaojiosayansi kutoka ndani na nje ya nchi unaofanyika Jijini Tanga
Alisema kuwa utafiti huu utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania na utasaidia kupunguza gharama za kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.
Bonde la Eyasi-Wembere linapita katika mikoa mitano ya Shinyanga, Simiyu, Arusha, Singida, na Tabora, ambapo lina uhusiano wa kipekee na maeneo mengine ya bonde la Ufa kama vile Uganda na Kenya, ambapo nchi hizo tayari zimegundua mafuta.
Maduhu aliongeza kuwa Tanzania ina matumaini makubwa ya kugundua mafuta kutokana na uhusiano huo na maeneo mengine ya bonde hili.
“Eneo hili ni muhimu sana kwa Tanzania kutokana na mshikamano wake na maeneo ya Lokicha nchini Kenya, ambapo mafuta yamevunjwa, na Uganda, ambapo wanajenga bomba la mafuta ghafi ili kupeleka mafuta hayo kwenye viwanda vya usafirishaji,” alisema Maduhu.
Kuhusu maendeleo ya Utafiti Maduhu alifafanua kuwa kazi za utafiti zimeendelea kwa hatua nzuri tangu kuanza kwa mradi huu mwaka 2015.
Alisema hadi sasa wamefanikiwa kukusanya taarifa muhimu zinazohusiana na uwepo wa mafuta katika eneo hilo. Alisema kuwa katika hatua hii, wanatekeleza uchukuaji wa taarifa za mitetemo za mifumo ya 2D ili kubaini maeneo ya kuchimba.
“Baada ya kuchora ramani ya mifumo ya 2D, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kujua kama mafuta yapo na kwa kiwango gani. Hadi sasa, Tanzania haijagundua mafuta, lakini tunatarajia kupata matokeo chanya kutokana na utafiti huu,” alieleza Maduhu.
Akizungumza umuhimu wa mradi huo kwa ajira, alisema kuwa kila awamu ya utafiti inahusisha watu 200,ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi ni Watanzania. Aliongeza kuwa uwepo wa rasilimali hii utachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha maisha ya Watanzania na kukuza uchumi wa taifa.
Alisema kwamba wanaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaunga mkono katika juhudi hizo pamoja na rasilimali hizo na watakuwa na nafasi nzuri ya kujikwamua kiuchumi na hatimaye kuwa miongoni mwa mataifa yaliyoendelea kiuchumi.
Akizungumza Mafanikio ya TPDC,Maduhu alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limepiga hatua kubwa tangu lilipoanzishwa katika miaka ya 1960.
Maduhu alitaja kuwa utafiti wa gesi na mafuta umeleta mafanikio makubwa, na kwa sasa TPDC inaendelea na utafiti wa mafuta ili kuongeza kipato cha taifa na kuleta maendeleo zaidi.
TPDC pia inaendelea na shughuli za uchimbaji wa gesi asilia, ambayo inachangia katika uzalishaji wa umeme na matumizi mengine ya nishati, na hivyo kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka nje, jambo ambalo linasaidia kupunguza athari za kimazingira. CODE