KIKOSI cha Simba kikiwa kamili gado, kimetua salama huko Algeria, huku benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na wachezaji wakiwa na hesabu moja tu dhidi ya Waarabu watakaovaana nao wikiendi hii nchini humo.
Simba inatarajiwa kuwa wageni wa CS Constantine inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Algeria, katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya awali kutakata nyumbani na ushindi wa bao 1-0 dhidi Bravos ya Angola.
Licha ya hali ya hewa ya Algeria kuwa ya baridi kali, lakini kikosi cha Simba kimetua kimkakati nchini humo, huku ikitamba wachezaji wote wana mzuka mwingi kuwakabili wenyeji wao katika mechi hiyo itakayopigwa Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku.
Simba ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Bravos do Santos ya Angola, ilitua juzi usiku ikiwa kamili gado kimkakati ili kuhakikisha inatoka na ushindi ugenini na Ofisa Habari wa timu hiyo akisema kila kitu kipo sawa na wachezaji wanaitaka sana mechi hiyo ili wajiweke pazuri katika msimamo wa kundi hilo.
Akizungumzia akiwa nchini humo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema wanashuruku hali ya wachezaji kiujumla ni njema, licha ya kusafiri kwa takribani saa 24, wakiwa angani kutoka Tanzania hadi Algeria unapochezwa mchezo huo.
“Tumefika jana usiku wa saa 4:00 kwa hapa Algeria ambayo ni saa 6:00 kwa Tanzania, tulitoa nafasi kwa wachezaji kuweza kupumzika na leo (jana) saa 9:30 ndipo kikosi chetu kitaanza maandalizi ya mchezo wetu wa Jumapili na CS Constantine,” alisema Ahmed na kuongeza wachezaji wote wana morali kubwa.
Ahmed alisema, hali ya hewa ni baridi kali kwa Algeria tofauti na Tanzania ndio maana waliamua kufika mapema ili kutoa nafasi kwa wachezaji kuweza kuzoea mazingira vizuri, ili wasiathirike kisaikolojia kabla ya kupambana na wapinzani wao.
“Licha ya hali hii ya baridi kali, lakini wachezaji wote na benchi la ufundi wapo katika hali nzuri na wanautaka mchezo huo, ili kuendelea paler walipoishia Kwa Mkapa,” alisema Ahmed.
Simba iliondoka na msafari wa watu zaidi ya 30 wakiwamo wachezaji 22 na itashuka uwanjani saa 1:00 usiku wa Jumapili kutupa karata ya mchezo wa kwanza ugenini wa kundi hilo kabla ya kurejea Kwa Mkapa wiki ijayo kuvaana na CS Sfaxien ya Tunisia.
Simba iliyofika robo fainali ya michuano hiyo misimu mitatu iliyopita ikitolewa kwa penalti na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, huku ikibebwa na rekodi tamu ya michuano ya CAF, ikicheza makundi katika misimu mitano kati ya sita, ikifika pia robo fainali yua Ligi ya Mabingwa ikiwamo msimu uliopita.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Simba, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limemteua mwamuzi wa kati, Godfrey Nkhakananga raia wa Malawi kusimamia mchezo huo wa CS Constantine na Simba utakaopigwa Jumapili.
Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Chahid Hamlaoui, unazikutanisha timu hizo zilizoshinda mechi zao za awali za Kundi A, huku refa huyo Mmalawi akipewa nafasi ya kupuliza kipyenga akiwa katikati.
Rekodi za mwamuzi huyo zinaonyesha hii itakuwa mechi yake ya kwanza kuchezesha Kombe la Shirikisho Barani Afrika hatua ya makundi, ingawa alishachezesha mechi za awali kusaka tiketi hiyo na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Nkhakananga amechezesha michezo mitano ya kimataifa ambapo rekodi zinaonyesha timu za nyumbani zimeshinda mara mbili, sawa na zile za ugenini huku sare ikiwa mechi moja tu, jambo linaloweza kuipa Simba faida ya kujiamini ikicheza ugenini.
Mchezo wa kwanza kuchezesha ulikuwa wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya awali ulioisha kwa sare ya kufungana bao 1-1, kati ya AS Kigali ya Rwanda dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, mechi iliyopigwa jijini Kigali Rwanda Februari 20, 2021.
Baada ya hapo Nkhakananga akachezesha tena michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya awali kati ya Maestro United Zambia (MUZA) ya Zambia iliyoichapa Cano Sport ya Equatorial Guinea mabao 3-0, mechi ambayo ilichezwa Agosti 27, 2023.
Mchezo uliofuata ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali pia ambapo alichezesha Bumamuru FC ya Burundi iliyochapwa mabao 4-0, dhidi ya Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini, mechi iliyopigwa jijini Bujumbura Burundi Septemba 15, 2023.
Nkhakananga akaendelea tena kuaminiwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwani alichezesha pia hatua ya awali mchezo kati ya AS Garde Nationale Nigerienne ya Niger iliyochapwa mabao 2-1, dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, mechi ikipigwa Agosti 17, 2024.
Mchezo wa mwisho kuchezesha ulikuwa pia wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali kusaka tiketi ya kutinga makundi kati ya Al Hilal ya Sudan iliyoichapa bao 1-0, FC San Pedro kutoka Ivory Coast, mechi ambayo ilichezwa Septemba 22, 2024.
Katika michezo hiyo yote mitano, rekodi zinaonyesha Nkhakananga ambaye pia ni mwalimu wa elimu ya viungo ametoa kadi za njano 14, akiwa na wastani wa kutoa kadi tatu kwa kila mchezo, huku jambo nzuri kwake hajatoa kadi yoyote ile nyekundu.
Simba ilifika makundi baada ya kuitoa Al Ahli Tripoli ya Libya kwa jumla ya mabao 3-1, baada ya kutoka suluhu mechi ya kwanza ugenini, kisha kupindua meza kibabe Kwa Mkapa kwa kushinda 3-1, huku Constantine ilianzia hatua za awali kwa kuitoa Police ya Rwanda kwa jumla ya mabao 4-1, kisha kukutana na Nsoatreman FC ya Ghana na kuitoa pia kwa maabao 3-0, ikishinda ugenini 2-0, kisha nyumbani bao 1-0.