Shinyanga. Wakati Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) likikabidhi eneo lililokuwa likitumiwa kutunza chakula kwenye maghala katika Kata ya Isaka wilayani Kahama mkoani humo Shirika la Reli Tanzania (TRC) na uongozi wa Kati hiyo wameomba kumilikishwa eneo hilo.
Eneo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 29,450 lilikuwa likitumiwa na WFP tangu 1996 hadi mwaka huu kusambaza chakula kwenye kambi za wakimbizi zilizopo Kenya, Uganda Rwanda, Burundi, DR Congo na Sudani Kusini.
Akizungumza jana Desemba 5, 2024 wakati wa kukabidhi eneo hilo kwa Serikali Naibu Mkurugenzi wa WFP, Christine Mendez amesema eneo hilo lilikuwa likihifadhi na kusambaza maharage, mahindi na mtama kwenda kwenye mataifa hayo.
Amependekeza Shirika la Reli likabidhiwe eneo hilo.
“Kituo hicho kilijengwa bure na WFP na kuweka mtandao wa miundombinu ya reli mbili za kutoka Stesheni ya Isaka hadi kwenye kambi hiyo iliyopo umbali wa mita 1,200, waliweka maghala 54 ya kuhamishika, uzio, nyumba mbili za watumishi na mashine,” amesema.
Ameongeza kuwa “Hivyo tunapendekeza eneo hili kama itawezekana wapatiwe Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwani shughuli ambazo tulikuwa tukizifanya baadhi zinahusiana na utunzaji wa mizigo kwa ajili ya usafirishaji, kwa hiyo naamini linaweza kuwafaa sana, alisema”
Baada ya kukabidhiwa eneo hilo kwa Serikali ya Halmashauri ya Kahama, Shirika la Reli na uongozi wa Kata ya Isaka wote wameonyesha nia ya kulitaka eneo hilo ambalo lina manufaa makubwa kiuchumi, endapo likitumika vizuri.
“Asilimia 70 ya uchumi wa Isaka ulijengwa na WFP na wao walikaa kwenye halmashauri na kujadiliana kuhusu eneo hilo, walipendekeza lilirudi kwenye Kata ya Isaka ili waweze kuweka miundombinu kama shule, ikiwezekana tugawane eneo na SGR” alisema Pazi Majuta, Diwani wa Kata ya Isaka
Meneja wa TRC kanda ya Tabora, John Mamuya amesema anaiomba Serikali ya Kahama iwapatie hilo eneo kwa ajili ya matumizi ya Shirika la Reli.
“Eneo hili tunapendekeza tupatiwe sababu hata katika ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) tutalitumia kuhifadhi vifaa na reli ikikamilika litatumika kuweka mizigo inayotarajiwa kusafirishwa,” amesema Mamuya
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo, Katibu Tawala Wilaya ya Kahama, Mohamed Mbega amesema watakaa vikao na uongozi wa juu kujua nani apewe umiliki wa eneo hilo.
“Tumekabidhiwa badala ya kazi waliyokuwa wakifanya WFP kumalizika, ajira zilitolewa na ulinzi kuimarishwa na mapendekezo yote yatajadiliwa kwenye vikao ndivyo vitakavyoamua mmiliki wa eneo hili,” alisema Mbega