Dar es Salaam. Tanzania imesaini mikataba minne ya mkopo nafuu na msaada wa jumla ya Sh327.9 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo awamu ya pili ya uzalishaji umeme wa jua wilayani Kishapu.
Kati ya fedha hizo, Sh8.281 bilioni ni msaada kwa ajili ya kufadhili mpango kazi wa Jinsia wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) chini ya mradi wa uendelezaji wa nishati ya jua.
Mikataba hiyo imesainiwa leo Desemba 6, 2024 jijini hapa baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo ya Ufaransa (AFD).
Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema mkataba wa kwanza utahusisha Sh209.52 bilioni kwa ajili ya mradi wa uzalishaji wa umeme jua awamu ya pili unaotekelezwa eneo la Kishapu mkoani Shinyanga.
Mkataba wa pili ni mkopo nafuu wa Sh110.147 bilioni kwa ajili ya mradi wa uendelezaji wa misitu na utunzaji wa hifadhi ya misitu ya mikoko.
“Katika mradi wa uendelezaji wa nishati ya jua hii ni awamu ya pili, mradi huu unatekelezwa kwa awamu mbili zenye jumla ya megawati 150. Awamu ya kwanza mkopo wake ulisainiwa Juni 11 2021 na upo katika hatua za utekelezaji na unatarajiwa kuzalisha megawati 50 utakapokamilika,” amesema Dk Mwigulu.
Amesema chini ya mkataba uliosainiwa Juni 11, 2024, AFD ilitoa mkopo nafuu wa Sh358.878 bilioni na kati ya fedha hizo Sh118.7 bilioni zinatumika kutekeleza awamu ya kwanza ya mradi huo wa nishati ya jua.
“Hivyo mkataba uliosainiwa leo kwa ajili ya awamu ya pili ni muhimu sana kwa kuwa utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huu inatarajiwa kuzalisha megawati 100 na kufanya jumla ya megawati zitakazozalishwa kuwa 150,” amesema Dk Mwigulu.
Mradi huu unalenga kufikia azma ya Serikali ya kuzalisha nishati mchanganyiko ukihusisha nishati jadidifu hadi kufikia mwaka 2025 kwa kutumia fursa ya kuwepo kwa vyanzo vya nishati tofauti hapa nchini.
Hilo litasaidia kuingiza megawati 150 kwenye gridi ya taifa zitokanazo na umeme jua, jambo ambalo litapunguza utegemezi wa umeme unaozalishwa na maji, ambao unaweza kuathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Kuhusu mkataba kwa ajili ya uendelezaji wa mashamba ya misitu na utunzaji wa hifadhi ya mikoko amesema unalenga kuongeza wigo wa upandaji miti, kuboresha ubora na wingi wa mbegu za miti na kuboresha usimamizi wake.
Jambo hilo litaimarisha vituo vya kukusanya mbegu za miti na kuanzisha vitalu vya kisasa vya miti.
“Utekelezaji wa mradi huu utaboresha utunzaji wa hifadhi ya misitu ya mikoko, kuboresha uhifadhi wa uhalisia wa mazingira na kuchangia kuinua utalii na kuboresha maisha ya jamii,” amesema Dk Mwigulu.
Naibu Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Axel-David Guuillon amesema miradi iliyopata fedha inaendana na vipaumbele vya ushirikiano vilivyowekwa kati ya nchi hizi mbili.
“Ingawa miradi hii inaonekana kuwa tofauti, kwa hakika ina mshikamano wa pamoja kwani inachangia kuunda mustakabali wa Tanzania kuelekea maendeleo zaidi, lakini kwa njia endelevu na shirikishi,” amesema Guuillon.
Ameongeza kuwa: “Miradi hii inashughulikia mahitaji ya wananchi kwa nishati na kuboresha maisha, huku ikikabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa mifumo ikolojia”
Awali akizungumzia fedha walizozipata kwa ajili ya uendelezaji misitu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Kitandula Dunstan amesema fedha hizi pia zitasaidia usimamiaji wa miti ya mikoko ambayo inafyonza hewa ya ukaa kwa kiasi kikubwa.
“Pia msaada huo utaimarisha jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kupata rasilimali zinazoweza kusaidia ustawi wa nchi, kwani itakuwa na uwezo wa kufyonza tani milioni mbili za hewa ya ukaa kwa mwaka na ikiingiza Sh25 bilioni kwa mwaka kwa kuuza hewa hiyo,” amesema Kitandula.